Breaking

Wednesday 13 July 2022

HALMASHAURI KALIUA YAREJESHA ZAIDI YA MIL 848 ZA MIKOPO



Na Lucas Raphael,Tabora

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 848.9 za marejesho ya mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani iliyotolewa na halmashauri hiyo kwa vikundi zaidi ya 70.

Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua mafanikio ya utekelezwaji agizo la Waziri Mkuu kwa halmashauri zote kuhakikisha fedha za mikopo zinazotolewa zinarejeshwa.

Alisema licha ya kuendelea kutekeleza agizo la serikali la kuwezesha vikundi vyote vya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu mikopo nafauu isiyo na riba, pia wameweka mkakati wa kufuatilia urejeshwaji mikopo hiyo ili vikundi vingi zaidi vinufaike.

Alibainisha kuwa hadi sasa jumla ya shilingi 848, 922, 050. zimesharejeshwa ambapo vikundi vya wanawake pekee vimerejesha kiasi cha shilingi 534, 313, 050. vijana wamerejesha shilingi 300,425,000. na watu wenye ulemavu shilingi 14,184,000..

Mwaga alifafanua kuwa zoezi la ukusanyaji marejesho ya mikopo hiyo linaendelea katika vikundi vyote na sasa imebakia kiasi cha sh milion 647.2 kati ya zaidi ya shilingi bilion 1.5 zilizokopeshwa na halmashauri hiyo.

Aliongeza kuwa fedha zinazorejeshwa mbali na kuendelea kutolewa kwa vikundi vingine pia zimekuwa zikisaidia kutekeleza shughuli nyingine za kimaendeleo ikiwemo kukamilisha miradi inayokwama.

‘Nimeshaelekeza timu ya mapato kwa kushirikiana na Maofisa Maendeleo ya Jamii na Watendaji kuongeza kasi ya ufuatiliaji ili vikundi vyote vikamilishe marejesho ya mikopo yao kwa wakati’, alisema.

Mwaga aliongeza kuwa mbali na kuendelea kutoa mikopo hiyo halmashauri ina mkakati wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki kupitia fedha hizo na zile za mapato ya ndani, hivyo akavitaka vikundi vyote kurejesha kwa wakati.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jafael Lufungija alibainisha kuwa ili kufanikisha mkakati huo wamepeleka timu ya watalamu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi kujifunza namna ya kuanzisha na kuendesha kiwanda hicho.

Alibainisha changamoto iliyopo kuwa ni baadhi ya vikundi kutorejesha mikopo yao kwa wakati ila akasisitiza kuwa wataendelea kuvifuatilia ili virejeshe fedha hizo huku akiongeza kuwa vitakavyokaidi vitafikishwa mahakamani.



Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages