Breaking

Friday 8 July 2022

LNG KUANZA UZALISHAJI WA GESI 2030



Na Selemani Msuya

MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema iwapo hakutakuwa na vikwazo, uzalishaji wa Mradi wa Kuchataka Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) katika Mkoa wa Lindi utaanza mwaka 2025 na gesi ya kwanza itaanza kuuzwa 2030.

Mhandisi Sangweni aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya 46 maarufu Sabasaba yanayofanyika katika Kiwanja cha Mwalimu Julius Nyerere Temeke Dar es Salaam.

Alisema kilichofanyika Juni 11 mwaka huu ilikuwa ni makubaliano ya awali ya mkataba husika, kama majadiliano ya muundo wa mradi, ukubwa wa mradi, sheria iweje na kwamba majadiliano yakikamilika wanatarajia Desemba 8 mwaka huu watasaini mkataba uliokamilika.

Sangweni ambaye ni Mwenyekiti wa Majadiliano alisema baada ya mkataba rasmi kukamilika wanatarajia kwenda kwenye kazi ya usanifu wa mradi na namna ya kupata fedha za utekelezaji.

“Tunategemea utekelezaji wa mradi huu ujenzi wake utaanza 2025 na ndani ya miaka minne hadi mitano utakuwa umekamilika na gesi ya kwanza itaanza kutoka 2030,” alisema.

Mhandisi huyo alisema iwapo hakutakuwa na changamoto katika mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh.trilioni 70 utaweza kuzalisha gesi asilia kwa miaka 30.

Alisema katika kipindi cha ujenzi wa mradi huo zaidi ya ajira 10,000 zitapatikana na ajira za kudumu zitakuwa zaidi 600 pamoja na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi kwenye eneo la mradi.

Mkurugenzi huyo alisema tafiti zinaonesha kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa kama hiyo ikifanyika katika nchi kama Tanzania pato la taifa litaongezeka kwa asilimia 1.5.

“Huu sio mradi mdogo, wakubeza, kwani utachangia ukuaji wa uchumi kwa kasi kubwa na pato la taifa litaongezeka kwa asilimia 1.5, ndio maana timu ya Serikali hailali kuhakikisha mradi unatekelezwa,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya mradi huo kuanza kuzalisha gesi asilia wanatarajia kuuza katika nchi za Mashariki ya Mbali kama Japani, China na nyinginezo ambazo zimeonekana kuhitaji.

Aliwataka wawekezaji wa Kitanzania na wengine kujipanga vizuri katika kutumia fursa zitakazokuwepo katika mradi huo, akitolea mfano kuwa nondo, saruji na bidhaa nyingine zitahitajika.

Mwenyekiti huyo alisema watajitahidi kuandaa mazingira wezeshi ili Watanzania wawe kwenye viwango ambavyo vinakubalika katika miradi mikubwa kama hiyo.

Alisema wamekuwa wakkifanya mikutano na wadau mbalimbali kama wakuu wa taasisi waweze kujiandaa kushiriki katika mradi huo ambao unaenda kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo.

Mkurugenzi huyo alisema azo la mradi huo lilinza mwaka 2012 ila kuna changamoto zilizotokea, lakini kwa sasa Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kuendeleza na matarajio yao ni mradi kutekelezwa kwa viwango vinavyokubalika.



Alisema kazi ya PURA ni kushauri Serikali kuhusu shughuli za mkondo wa juu, kuthibiti na kusimamia Mradi wa LNG ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania.

Sangweni alitoa wito kwa Watanzania kutembelea banda la PURA ili waweze kupata elimu zaidi kuhusiana na mamlaka hiyo ambayo ina kazi moja ya kuhakikisha rasilimali mafuta na gesi zinagundulika na kutumika.

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages