Breaking

Monday 25 July 2022

MBUNGE KABULA KUCHANGIA MATOFALI 400 KILA WILAYA MWANZA KUJENGA MADARASA, AANZA NA MISUNGWI



Katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwenye mazingira rafiki na salama Mkoa wa Mwanza umeanzisha kampeni ya kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa inayoitwa ' uzalendo kwanza kazi iendelee. '

Kampeni hiyo imezinduliwa leo jumatatu ya Julai 25, 2022 katika Kijiji cha Mbela kilichopo Wilaya ya Misungwi Mkoani hapa.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mbunge viti maalumu Mkoa wa Mwanza Kabula Shitobelo, amesema wazazi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuwapeleka watoto wao shule hivyo kufanya idadi ya wanafunzi kuwa kubwa ukilinganisha na vyumba vya madarasa vilivyopo.

"Kupitia kupitia kampeni hii nitasaidia tofari 400 kila Wilaya zitakazosaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa" Amesema Mbunge Kabula

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, amesema kampeni hiyo ya kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa ina thamani ya Bilioni 238.08.

Amesema watanzania wanapaswa kuwa wazalendo kwa kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuchimba msingi, kusomba mawe ili kuweza kupunguza gharama zitakazosaidia katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Katika kampeni hiyo Mbunge wa Jimbo la Misungwi Alexander Mnyeti amechangia Milioni 20 kwaajili ya kuunga mkono ujenzi wa vyumba 25 vya madarasa katika shule ya mbela.



Amesema shule ya Mbela ina watoto wengi kuliko shule zote zilizoko kwenye wilaya hiyo, uwezo wa shule ni kubeba wanafunzi 800 lakini idadi ya wanafunzi waliopo kwenye shule hiyo ni 2000 hivyo ujenzi wa Madarasa hayo yatakuwa suluhisho la kudumu na itasaidia wanafunzi kusoma vizuri.

Naye Mkuu wa wilaya ya Misungwi Veronica Kessy, amewaomba wananchi kuendelea kujitolea katika kufanya kazi za kimaendeleo hali itakayosaidia watoto kusoma katika mazingira mazuri na hatimae kutimiza ndoto zao.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages