Breaking

Thursday 7 July 2022

MWANI KUKUTANISHA WADAU ZANZIBAR


Na Selemani Msuya, Dar Es Salaam


VIONGOZI, taasisi, wakulima na wadau mbalimbali wa zao la mwani wanatarajiwa kukukutana katika Kongano Bunifu la Mwani Zanzibar (Zasci) kuanzia Julai 23 mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Zasci, Rajab Ally Ameir wakati akizungumza na mwandishi wa habari katika maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika kwenye Viwanja vya Julius Nyerere Sabasaba wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.

Alisema wana Kongano la Mwani Zanzibar tangu kuanzishwa wamekuwa wakikutana siku moja kwenye mwaka na kujadili namna ya kusukuma sekta hiyo muhimu kwa uchumi wan chi.

Ameir alisema matarajio yao ni kongano hilo kushirikisha viongozi, wakulima, wazalishaji, Tume ya Tafa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

Alisema kongano hilo lilianzishwa kwa msaada wa COSTECH kwa ajili ya kusadia kutatua changamoto za wakulima wa mwani baada ya kuonekana hawafaidiki na kilimo hicho.

Katibu huyo a alisema wanatarajia kupata wageni kutoka maeneo kama Mombasa, Tanga, Bagamoyo, Mafia, Pemba na Ugunja ambapo ni Ukanda wa Bahari ya Hindi.

“Julai 23 wana Kongano la Mwani tutakutana Zanzibar kujadiliana kuhusu zao hili ambao lina faida nyingi za kiuchumi, kijamii, afya na maendeleo. Nitumie nafasi hii kuwakaribisha wadau wote wanaojihusisha na zao hili,”alisema.

Katibu huyo alisema kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuuza mwani duniani ikiongozwa na Philippine na Indonesia, hivyo juhudi zao kama kongani ni kuhakikisha inaongoza.

Alisema hadi sasa kuna wakulima zaidi ya 24,000  wa zao la mwani ambapo asilimia 80 wanatoka Pemba na 20 Unguja huku wanawake wakiwa asilimia 80.

Ameir alisema mikakati yao ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wote ambao wapo katika Ukanda wa Bahari ya Hindi ili waweze kushiriki kulima mwani kwani ni zao ambao soko lake ni la uhakika.

Alisema matarajio yao ni kuona zao hilo linachangia ukuaji wa uchumi Zanzibar na Tanzania Bara kama yalivyo mazao mengi, hasa kwa kukuhakikisha kuwa linachakatwa hapahapa nchini.

Ameir alisema kwa sasa asilimia 2 ya mwani ndio inachakatwa nchini, huku asilimia 98 ikiizwa kama malighafi hali ambayo inasababisha bei kuwa chini.

Katibu huyo alipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuamua kujenga kiwanda cha kuchakata mwani huko Chamangwena Pemba na kuwaomba wadau wengine waanzishe viwanda.

Alisema mikakati yao ni kuhakikisha mwani unatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo Karajinan, Aga na vingine ambavyo vitaongeza mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Mwisho.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages