Breaking

Wednesday 20 July 2022

SUMA JKT YATAKIWA KUKABIDHI JENGO LA OFISI ZA KARAKANA YA NDEGE JULAI 31, 2022



Na Veronica Mwafisi, Dar es Salaam

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Mkandarasi SUMA JKT kuhakikisha anakabidhi jengo la ofisi za karakana ya ndege (HANGAR) kwa Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA) tarehe 31 Julai, 2022, ili kuiwezesha TGFA kuongeza ufanisi katika kutoa huduma ya usafiri wa anga kwa viongozi wakuu wa nchi wakiwa katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ofisi za karakana ya ndege na kuridhika na hatua iliyofikiwa.

Mhe. Ndejembi amesema ofisi yake inategemea tarehe 31 Julai, 2022 jengo la Ofisi ya Karakana ya Ndege litakabidhiwa kwa TFGA, kwani TGFA inategemewa sana na Serikali katika kutoa huduma bora za usafiri wa anga kwa viongozi wakuu wa kitaifa.

“Baada ya kufanya ukaguzi, nimeridhika na kiwango cha ubora na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na mkandarasi katika ujenzi wa jengo hili la ofisi za karakana ya ndege,” Mhe. Ndejembi amefafanua.


Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama anawapongeza Mkandarasi SUMA JKT, Mshauri Mwelekezi DIT na Mzabuni TGFA kwa ujenzi uliozingatia ubora.

“Tumeona namna jengo lilivyo la kisasa, kwani limewekewa vifaa vya kupambana na moto ikiwa ni pamoja na kuwezesha matumizi mazuri ya umeme,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ndege za Serikali (TGFA), Mhandisi John Nzulule amemshukuru Waziri Jenista Mhagama na Naibu wake Mhe. Deogratius Ndejembi pamoja na wajumbe wa bodi, kwa kufanya ziara za kukagua maendeleo ya ujenzi katika nyakati tofauti, lengo likiwa ni kuhimiza ukamilishaji wa ujenzi wa ofisi za karakana ya ndege ambao hivi sasa upo katika hatua nzuri kutokana na ufuatiliaji wao.

Kukamilika kwa jengo la ofisi za karakana ya ndege (HANGAR) kutaiwezesha TGFA kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages