Breaking

Wednesday 13 July 2022

WATU WATANO WAFARIKI, 11 WAJERUHIWA AJALI YA GARI SIMIYU




Watu watano wamefariki dunia na wengine 11 wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Magereza nje kidogo ya mji wa Bariadi Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu usiku wa kuamkia leo Julai 13, 2022.

Ajali hiyo imetokea siku moja baada ya ajali nyingine kusababisha vifo vya watu wanane wakiwamo watano wa familia moja iliyotokea katika barabara kuu ya kutoka Lusahunga kwenda Nyakahura wilayani Biharamulo Mkoani Kagera baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso.


Kamanda wa Polisi Mkoa Simiyu, Blasius Chatanda amesema kuwa ajali hiyo imehusisha magari madogo ya abiria.

RPC mkoa wa Simiyu amethibitisha vifo hivyo na kusema "Nimefika eneo la ajali nimeona waliofariki wote ni wanaume. Gari moja mchomoko lilikuwa likitokea Lamadi na lingine Bariadi. Dereva aliyekuwa akitoka Lamadi aliova-take ndipo akakutana na mwenzake. Chanzo ni mwendo kasi. Madereva wamejeruhiwa na wapo chini ya ulinzi,"


Akizungumza na waandishi wa habari usiku wa kuamkia leo, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya mji wa Bariadi, Somanda Emmanuel Constantine amethibitisha kupokea miili ya watu wanne na majeruhi wanne.

“Majeruhi tuliowapokea wamepata majeraha kwenye migongo na hali zao zinaendelea vizuri na hadi sasa wanaendelea kupatiwa matibabu hapa hapa hospitalini” amesema Dk Constantine.

Ajali hiyo ilihusisha magari madogo mawili ya abiria aina ya Toyota pro box na Toyota wish ambayo yanayofanya safari zake kati ya mji wa Bariadi na Lamadi wilayani Busega ambayo yaligongana uso kwa uso.

Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya magonjwa ya dharura katika Hospital ya rufaa ya mkoa wa Simiyu, Dk Seleman Athuman amesema alipokea majeruhi wanane ambapo baadhi yao wamevunjika katika baadhi ya viungo na mmoja alifariki wakati anatibiwa na kufanya idadi ya vifo kuwa watu watano.


“Tulichokifanya cha kwanza tumewapatia huduma ya kwanza kuwatoa katika hali ya dharura na kuwaweka katika hali ya utayari kwa kuendelea kupata matibabu zaidi katika Hospital ya Rufaa ya Kanda ya Bugando,” amesema Dk Athuman.

Ajali hii inatokea ikiwa ni siku 13 tangu kutokea kwa ajali nyingine ya gari aina Toyota wish iliyopata ajali eneo la Luguru wilaya ya Itilima mkoani humo kuua watu watano huku ikijeruhi wengine watano.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages