Breaking

Sunday 17 July 2022

WIZARA YA NISHATI KUPITIA REA WAJA NA MABADILIKO MAPYA, WALEGEZA MASHARTI YA UJENZI VITUO VYA MAFUTA VIJIJINI



Na Lydia Lugakila, Lango la habari

Waziri wa Nishati January Makamba amesema kuwa wizara kupitia wakala wa umeme vijijini -REA italeta mabadiliko ya kulegeza masharti ya ujenzi wa vituo vya mafuta ya petroli lengo ikiwa ni kuondoa changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta.

Kauli hiyo ameitoa julai 15, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Nyakanazi lililopo wilayani Biharamulo Mkoani Kagera katika ziara ya kikazi inayolenga kusikiliza na kutatua changamoto na kero za wananchi katika masuala ya nishati jadidifu.

Waziri Makamba amesema kuwa wizara ya nishati kupitia wakala wa umeme vijijini -REA wanakuja na mabadiliko ya ulegezaji masharti ya ujenzi wa vituo vya mafuta ya petroli lengo likiwa ni kuondoa changamoto ya bei ya mafuta kuwa juu pamoja na kuondoa tatizo la utumiaji wa mafuta ambayo si safi yanayosababisha vyombo vya usafiri kuharibika.

"Watu wa vijijini wanapata shida hasa boda boda wananunua mafuta kwa bei ya juu, wananunua mafuta kwenye vidumu na kwenye vichupa vya maji, mafuta yanakuwa si safi kwani yameishahama kutoka kwenye vyombo zaidi ya vinne kutoka kwenye pampu" alisema waziri Makamba.

Amesema mafuta yaliyo mengi uning'inizwa juani kutwa nzima na kupoteza ubora wakati mwingine mtu akinunua mafuta kwenye chupa anapunjwa.

Akieleza namna masharti ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini yatakavyokuwa amesema badala ya mtu kujenga kituo cha mafuta ambacho mtu anaweka paa kubwa la zege kwa juu na gharama inakuwa kubwa hadi kufikia milioni 200 hadi 300 sasa masharti yamerahisishwa kwa vituo vya mafuta vijijini.

"tunataka uweke bati la kawaida badala ya zege iliyoenda juu, hatuhitaji uwe na hati, kikubwa serikali ya Kijiji iwe imekuruhusu hivyo tumeshusha gharama hizo hadi milioni 40 ambapo tumeweka mpango wa kukopesha pesa kwa mtu yeyote "alisema waziri huyo.

Akitolea majawabu katika baadhi ya changamoto zinazoikabili wilaya ya Biharamulo zilizowasilishwa na mkuu wa wilaya hiyo Bi Kemilembe Lwota juu ya baadhi ya wananchi kulalamikia kucheleweshewa kufungiwa umeme licha ya kuwa walishalipia muda, waziri amesema tayari wameagiza vifaa vingi na kufikia oktoba 15, 2022 hakutakuwepo na mtu aliyeomba hajafungiwa umeme.

Aidha akizungumza bei ya umeme kwa wakazi wa Nyakanazi ambao hawajafungiwa umeme amesema itabaki kuwa shilingi elfu 27 bila nyongeza huku wale wa mfumo mpya kuunganishiwa ndani ya siku 7 ambapo pia amewahimiza wananchi kutumia njia rahisi ya mfumo mpya wa maombi wa kuunganishiwa umeme uitwao NIKONEKT.

Pia Waziri Makamba ameahidi kumaliza tatizo la kukatika katika kwa umeme na kuwa tayari shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa kushirikiana na wizara ya nishati wanatarajia kuifanya Nyakanazi kuwa na kituo kikubwa cha mfumo wa gridi ya Magharibi ya Tanzania.

Katika hatua nyingine Waziri makamba amepokea ombi la Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mhandisi Ezra Chiwelesa la kuwawekea taa za Barabarani katika eneo la Nyakanazi ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kufanya Biashara zao nyakati za usiku.

Mbunge wa Jimbo la Biharamulo amemwambia Waziri Makamba kuwa Nyakanazi ndiko yanayopitia magari yote yanayoenda katika nchi za Uganda , Rwanda ,Burundi na Kongo kutoka Bandari ya Dare es salaam lakini hakuna usalama wa Biashara nyakati za usiku Jambo linalopelekea wafanyabiashara Kufunga mapema ili kuepukana na wizi.

Hata hivyo Makamba amesema serikali inashughulikia haraka swala la kufunga taa za Barabarani katika eneo la Nyakanazi na kuweka Uhuru wa kibiashara kwa masaa 24.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages