Breaking

Saturday 16 July 2022

WAZIRI BASHUNGWA AAGIZA MAENEO YA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI KUPIMWA




Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha maeneo ya Shule zote za Msingi na Sekondari yanapimwa na kupatiwa hatimiliki.

Mhe. Bashungwa ametoa agizo hilo Julai 15, 2022 alipofanya ziara kwenye Shule ya Sekondari Ndama iliyopo Wilaya ya Karagwe na kubaini shule hiyo kutokuwa na hatimiliki ya shule hali inayosababisha kuwapo kwa uvamizi wa maeneo ya shule na taasisi nyingine za Serikali.

“Nawaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha Shule zote za Msingi na Sekondari nchini nzima zinapimwa na kuwa na hati ya maeneo yake,” amesema Mhe.Bashungwa.

Aidha, Mhe.Bashungwa baada ya kusikiza changamoto za Shule hiyo, amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/23 Serikali italeta fedha kujenga maabara ya Baiolojia na Fizikia katika shule hiyo ili wanafunzi wapate masomo kwa vitendo.

Hata hivyo, Waziri Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kupeleka Sh.Milioni 30 zilizokuwa zimetengwa na Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa maabara, ili fedha hizo zitumike kujenga jengo la utawala katika Shule hiyo.

Vile vile, Amemuagiza Mkurugenzi huyo kutenga fedha na kuweka kipaumbele cha ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule hiyo kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri na akasisitiza halmashauri zote nchini kutekeleza maelekezo hayo.

Waziri huyo pia, Amemuagiza Meneja wa mradi wa maji mjini (BUWASA) wilayani humo, kuhakikisha mabomba ya maji katika mradi wa maji unaotekelezwa katika Mji Mdogo wa Kayanga, yanafikishwa kwenye shule hiyo ili wanafunzi waondokane na changamoto ya kufuata maji nje ya mazingira ya shule.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages