Breaking

Friday 19 August 2022

SHAKA AAGIZA KUCHUKULIWA HATUA MTENDAJI WA KIJIJI KALIUA



Na Lucas Raphael,Tabora

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka ameagiza Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora kumchukulia hatua aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Ibambo kata ya Mwongozo Adam Muyaga kwa tuhuma za ubadhirifu.

Ametoa agizo hilo jana baada ya kupokea malalamiko ya wananchi akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake wilayani humo ambapo alisikitishwa na uamuzi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kumhamisha kituo cha kazi badala ya kumchukulia hatua Mtumishi huyo.

Alisema haiwezekani Mtumishi atafune fedha zilizochangwa na wananchi kwa ajili ya kujiletea maendeleo halafu halmashauri imhamishe kituo cha kazi badala ya kumchukulia hatua stahiki ikiwemo kurejesha fedha alizochukua.

Alibainisha kuwa zaidi ya sh 900,000 zilichangwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya msingi Ibambo ili kumaliza tatizo la uhaba wa vyoo katika shule hiyo lakini cha kusitikisha Mtendaji huyo akaondoka nazo.

‘CCM haikubaliana na vitendo vya namna hiyo, Mkuu wa wilaya fuatilia hili, wasiliana na Mkurugenzi wa halmashauri, huyu Mtumishi arejeshe fedha zote na achuliwe hatua stahiki, na nipewe taarifa kabla sijaondoka hapa Tabora’, alisema.

Shaka alisisitiza kuwa kulea watumishi wanaofanya ubadhilifu ni kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi na kuongeza kuwa vyoo hivyo vimekwama kwa zaidi ya miaka 3 na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na mhusika yupo.

Aliongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anajali sana wananchi wake ndiyo maana ameleta fedha nyingi sana kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu, afya, maji na barabara, hivyo haitamfumbia macho Mtumishi yeyote atakayetumia vibaya fedha za maendeleo.

Diwani wa Kata ya Ilege ambaye ndiye Mwenyekiti wa halmshauri hiyo Japhael Lufungija alimweleza kuwa awali halmashauri ilitoa mifuko 190 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyoo hivyo lakini akashangazwa na usimamizi mbovu wa mradi huo.

Akitolea ufafanuzi suala hilo Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Keneth Kefurukwa alisema Mtendaji huyo ambaye alihamishiwa Kijiji cha Malanga Kata ya Usenye katika halmashauri hiyo bado hajaachiwa ila suala lake lilikuwa kwenye uchunguzi, hivyo akaahidi kuwa watalifanyia kazi.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages