Breaking

Friday 5 August 2022

RC CHALAMILA AKABIDHIWA MIKOBA KAGERA, AWAPA MANENO MAZITO WATUMISHI


Na Lydia Lugakila, Lango la habari, Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amekabidhiwa rasmi ofisi ya mkoa huo tayari kwa kuanza kazi huku akikemea makando kando na kubezana kwa watumishi jambo alilolitaja kuchelewesha maendeleo ya mkoa.

Rc Chalamila ameyaeleza hayo katika hafla ya makabidhiano kati ya mtangulizi wake Meja Jenerali Charles Mbuge iliyofanyika Agosti 4,2022 katika ukumbi wa Mkoa wa Kagera.

Rc Chalamila amesema kuwa hanaga kona kona katika kazi hivyo yupo tayari kuibadili Kagera kwa haraka endapo akipewa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watumishi ambapo pia amekemea kubezana katika kazi na kuoneana.

"Sisi tunafanya kazi ya sadaka kazi hii ni zawadi toka kwa Mungu nipo tayari kuifanya japo kuna watu waliopo kwa ajili ya utani na kubeza kile mtu amefanya tabia hii ni ya kuacha "alisema Rc Chalamila.

Aidha Chalamila ameahidi kuufungua Mkoa wa Kagera kiuchumi ikiwa ni pamoja na kushirikiana na nchi jirani ili kudumisha Diplomasia huku akimpongeza Rais Samia kwa kumteua katika nafasi hiyo.

Kwa upande wake aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Meja Jenerali Charles Mbuge amemuomba Chalamila kuhakikisha anasimamia zao la kahawa ili lisiyumbe ikiwa ni pamoja na kuzuia magendo, kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati na kuleta tija kwa wanakagera na taifa kwa ujumla.

"Karibu Kagera nimeacha mradi mkubwa wa bomba la mafuta, zao la kahawa nimeliacha katika hatua nzuri haya yote yaendelezwe ili kuleta maendeleo" alisema Meja Jenerali Charles Mbuge.

Naye katibu tawala wa Mkoa wa Kagera Toba Nguvila amemshukuru Rais Samia kwa kumteua ambapo ameahidi kuwatumikia wananchi Mkoani humo kwa kufanya kazi usiku na mchana.

Ameongeza kuwa suala la majungu likiwekwa pembeni upendo na ushirikiano vikiwekwa mbele Mkoa huo utakua kwa kasi kubwa.

Nguvila akimzungumzia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Meja Jenerali Charles Mbuge amesema alikuwa msaada mkubwa sana kwa watumishi wote, alisimamia vyema miradi ya maendeleo pamoja na kuonesha upendo kwa wana Kagera.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages