Breaking

Saturday 6 August 2022

WAZIRI MCHENGERWA AKUTANA NA UNESCO, AUNDA TUME UANZISHWAJI WA CHUO KIKUU CHA KISWAHILI

Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amekutana  na ujumbe wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na ameunda tume kwa ajili ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiswahili nchini ikiwa ni mkakati kabambe wa kubidhaisha lugha ya Kiswahili  katika  mabara yote duniani.

Mhe, Mchengerwa ameunda tume maalum ya uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Kiswahili kufuatia  ombi lake alilolitoa  kwa  shirika  la UNESCO wakati wa siku ya  maadhimisho ya Kiswahili duniani   mwaka huu iliyofanyika  kwa mara ya  kwanza  Julai 7, 2022. 

Akizungumza mara baada ya mkutano na ujumbe wa UNESCO ofisi za Tanzania leo Agosti 5, 2022 ofisini kwake jijini Dar es Salaam amesema matajio ya  Serikali ni kuona kuwa Kiswahili kinavuka mipaka  ya   Tanzania.

Aidha, Mhe Mchengerwa ameipa tume  hiyo siku  tano  kukamilisha andiko  hilo ili liwasilishwe kwenye  ngazi za juu kwa ajili ya maamuzi.

Amesema hadi sasa tayari Serikali imetenga na kutoa ekari mia  moja kwa ajili ya kujenga chuo hicho ambacho kinatarajiwa kuwa kitalu cha  kuzalisha, kuhifadhi na kuendeleza lugha adhimu ya Kiswahili   kwenye mataifa mbalimbali duniani.

Amesema katika kikao hicho pamoja na mambo mengine pia wamejadili namna ambavyo wanaweza kuendeleza na kukuza Kiswahili na kuwa nyenzo ya  kufundisha lugha ya Kiswahili kwenye lugha nyingine kubwa zakimataifa.

Amefafanua kuwa  uanzishwaji wa chuo kama hiki ni jambo ambalo limeshafanyika kwenye mataifa mengine  duniani  na kuleta  mafanikio makubwa hivyo hakuna sababu ya Tanzania kisiwepo, sehemu ambayo ndiyo chimbuko na kiini cha Kiswahili duniani 

Amesema   namna bora ya kubidhaisha Kiswahili ni kuwa na chuo maalum ambacho  kitajikita kwwnye kuendeleza lugha ya Kiswahili na  lugha ndogondogo ambazo zimekuwa zikisaidia  katika kutoa misamiati kadhaa  ya Kiswahili.

Aidha, amesisitiza kuwa chuo hicho kitasaidia kuhifadhi lugha nyingine ndogondogo ambazo zinakwenda kufa ambapo pia kitasaidia  kufanya utafiti wa kina kwenye eneo la Kiswahili na  lugha mbalimbali za kimataifa  ili mkakati wa kubidhaisha uweze  kufanikiwa. 

Kwa upande mwingine Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa lugha ya Kiswahili ni lugha mahususi iliyotumika katika ukombozi wa Bara la Afrika ambapo pia kutokana na umuhimu huo kuja haja ya kukienzi kwa kuwa na chombo maalum kitakachosaidia kuendeleza, kutunza na  kuhifadhi Kiswahili.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages