Breaking

Friday 16 September 2022

BASHUNGWA AWAPA MAAGIZO MADED, ATAKA SHULE KUWA NA HATIMILIKI YA ARDHI KABLA YA DISEMBA 30



Na OR TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia zoezi la shule zote, za msingi na sekondari zinapimwa na kuwa na hatimiliki ya ardhi ya maeneo yao kabla ya Disemba 30 mwaka huu.

Bashungwa ametoa maelekezo hayo leo Septemba 16, 2022 Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa majibu ya nyongeza katika maswali ya waheshimiwa wabunge kuhusu serikali kutenga maeneo ya kujenga miundombinu na viwanja vya michezo shuleni.

“Nimeshatoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha shule za msingi na sekondari nchini zinapima maeneo yao na yanakuwa na hatimiliki na nipate nakala hiyo ofisini kwangu kabla ya Disemba 30” amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo nchini, jambo ambalo ni moja ya kipaumbele cha serikali.

Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI inashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuendeleza sekta ya michezo ngazi ya Halmashauri.

“Nasisitiza maeneo yote ya michezo katika shule zote za msingi na sekondari kupimwa na kutambua maeneo ya michezo na kuyalinda ili yasivamiwe" amesisitiza Bashungwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages