Breaking

Thursday 22 September 2022

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AYAASA MATAIFA KUCHANGIA MFUKO WA GLOBAL FUND



Na Mwandishi Wetu 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa mataifa ulimwenguni kuungana katika kutoa mchango kwa mfuko wa kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) ili uweze kufikia lengo la kukusanya kiasi cha dola za kimarekani bilioni 18 zitakazotumika kutokomeza magonjwa hayo.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia Mkutano wa saba wa kuwezesha mfuko wa kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) uliofanyika New York nchini Marekani.

Amesema Migogoro ya sasa ya kimataifa imepunguza juhudi za kurejesha uchumi wa nchi nyingi ulioathirika na janga la UVIKO19 na kuongeza changamoto mpya katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu hivyo hakuna budi wote kwa pamoja kuona haja ya kuunga mkono kazi nzuri ya Mfuko huo wa Kimataifa ili kuendeleza mafanikio katika kukabiliana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.

Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo baina yake na Global Fund, ambao umekuwa na matokeo chanya yaliopelekea kupunguza idadi ya vifo kwa magonjwa ya Ukimwi ,Kifua Kikuu na Malaria.

Ameishukuru Bodi ya Global Fund kwa kuinga mkono Tanzania kwa miaka mingi pamoja na kuzishukuru na kuzipongeza Serikali, Mashirika, Taasisi na watu binafsi wote kwa michango yao kwa Mfuko huo kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imejitolea kufikia lengo la kimataifa la kukomesha ugonjwa wa Ukimwi ifikapo 2030 kwa kutumia teknolojia mpya na mikakati ya kibunifu.

Ameongeza kwamba licha ya mafanikio yaliopatikana katika kukabiliana na Ugonjwa wa Ukimwi , Kifua Kikuu na Malaria , bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya maambukizi mapya hususani kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24.

Pia amesema katika kukabiliana na Kifua Kikuu bado taifa linakabiliwa na vikwazo kama vile upatikanaji mdogo wa huduma za uchunguzi wa ugonjwa huo hasa katika maeneo yenye watu muhimu na walio hatarini ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa migodini, wavuvi na wafungwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages