Breaking

Friday 30 September 2022

RAIS SAMIA ATAKA VIONGOZI WALIOTUMIA VIBAYA FEDHA ZA LISHE WACHUKULIWE HATUA



Angela Msimbira TAMISEMI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa kuwachukulia hatua viongozi wote waliotumia vibaya fedha za lishe kufanyia mambo mengine badala ya kuzielekeza kwenye maswala ya lishe.




Rais Samia amesema hayo leo Septemba 30, 2022 Jijini Dodoma kwenye Hafla ya Utiaji Saini wa Mkataba ya Usimamiaji wa Shughuli za lishe na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ambapo amesema kuwa fedha zilizoelekezwa kwenye afua za lishe zifanye kazi zake kwa ufasaha katika maeneo yao.




“Kwa wale wote waliotumia vibaya fedha za lishe wachukuliwe hatua stahiki kwa kuwa huo ni utovu wa nidhamu na hii inaonyesha kuwa hata katika miradi mingine inafanyika hivyovyo, hili halikubaliki kabisa wachukuliwe hatua kali” amesema Rais Samia




Amemuagiza Waziri wa Nchi – TAMISEMI kuwasilisha taarifa ya Halmashauri zote ambazo zimetumia fedha za lishe katika kutekeleza miradi mingine ili hatua kali ichukuliwe kwa wahusika.




Amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia fedha zinazopangwa kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya lishe kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuhakikisha zinatolewa kwa wakati ili kutekeleza afua za lishe.




Amesema kuwa mpango wa lishe hautekelezwi ipasavyo, hivyo Wakuu wa Mikoa wahakikishe wanajipanga na kuongeza jitihada za kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za lishe bora na kupanga vipaombele ili kuleta tija




Aidha Rais Samia amesema kuwa Serikali itaweka nguvu zaidi kwenye uboreshaji wa huduma bora za afya katika Vituo vya Afya kwa kuwekeza kwenye ununuzi wa vifaa na vifaatiba, madawa, kuajiri watumishi pamoja na kujenga nyumba za watumishi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages