Breaking

Tuesday 18 October 2022

BIMA YA AFYA KWA WOTE HAITAKUA NA MATABAKA - WAZIRI UMMY



Na Emmanuel Malegi - WAF, Dodoma

Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Muswada wa bima ya afya unalenga kutoa huduma za matibabu kwa wananchi wote bila kujali tajiri au maskini hivyo hautakua na matabaka.

Waziri Ummy amesema hayo leo 18 Oktoba 2022 wakati akiwasilisha muswada huo mbele ya Kamati ya Kudumu ya huduma na Maendeleo ya Jamii kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema muswada huo bado haujapitishwa hivyo wizara inaendelea kupokea maoni kutoka katika makundi mbalimbali nchini ili kuweza kuiboresha na kuwa bima yenye manufaa kwa wananchi wote.

Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa huduma zitakazotolewa kwa mwananchi itategemea na michango yake aliyochanga katika kipindi fulani ili kuepuka kugharamia huduma zenye gharama kubwa kwa mgonjwa aliyechangia mwezi mmoja hivyo kupelekea mfuko kuteteleka na hatimaye kuanguka na kushindwa kutoa huduma, hivyo amewataka wananchi kujiunga na kuchangia mapema kabla ya kuugua.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kamati yake itakutana na wadau mbalimbali ili kupokea maoni yao kabla ya kutoa maoni ya jumla, lengo likiwa ni kuboresha muswada huo kabla haujapitishwa na kuwa sheria rasmi.

Mhe. Nyongo amesema lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake ili wawe na uhakika wa kupata matibabu pindi wanapougua hivyo muswada huo unatakiwa kupitiwa kwa uangalifu ili uguse wananchi wote bila kikwazo cha kiuchumi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages