Breaking

Saturday 15 October 2022

MAHAKAMA YABADILI HATI YA MASHITAKA, WAUAJI WAWILI WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA NJE





Na Lucas Raphael,Tabora

Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora kwa mara ya kwanza imebatilisha hati ya Mashitaka na kuwahukumu kifungo cha miezi 12 nje ya gereza washitakiwa wawili wa kesi ya mauaji baada ya kuwatia hatiani kwa kosa dogo la kuua bila kukusudia.

Uamuzi huo umefikiwa Octoba 13, 2022 na hakimu Mkazi wa mahakama ya Mkoa wa Tabora aliyekasimiwa Mamlaka ya ziada ,Jovitti Katto baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili.

Hakimu Katto alisema kwa kutumia Mamlaka aliyopewa na kwa kutumia kifungu namba 300 kifungu kidogo cha kwanza anabadilisha shitaka la mauaji na kuwa kosa dogo la kuua bila kukusudia.

Kifungu hicho cha sheria ya makosa ya jinai kinaeleza kuwa, Wakati mtu anashtakiwa na kosa na maelezo yanathibitisha kwa kupunguza kosa na kuwa kosa dogo, anaweza kutiwa hatiani kwa kosa hilo dogo japokuwa hakushtakiwa na kosa hilo.

Washitakiwa wa kesi hiyo ya mauaji ni Mrisho Ramadhani na mwanae Ramadhani Mrisho wakazi wa eneo la Kidatu kata ya Kiloleni Manispaaya Tabora.

Mara baada ya kubadili hati ya mashitaka hakimu Katto aliwatia hatiani washitakiwa wote kwa kosa dogo la kuua bila kukusudia ndipo akawahuku kifungo cha miezi 12 nje ya gereza ambapo aliwataka wawe wanafanya usafi eneo la mahakama.

Akichambua maelezo ya mashahidi wa kesi hiyo Hakimu Katto alisema kuwa Mahakama imejiridhisha kwamba Hussein Ibrahim ambaye kwa sasa ni Marehemu ndiye aliyejisababishia kifo chake kutokana na kuanzisha vurugu na kuwatolea matusi washitakiwa.

Awali upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili Robert Kumwembe ulidai kuwa Aprili 14/2020 usiku washitakiwa walimshambulia Hussein Ibrahimu na kumsababishia majeraha na alifariki kesho yake muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya kitete.

Akisoma hukumu hiyo hakimu alisema kuwa mahakama haina haja ya kujaza magereza na kwa kuzingatia utetezi wao kwamba miaka miwili waliyokaa mahabusu imekuwa funzo kwao watatumikia kifungo cha miezi 12 nje ya gereza.

MWISHO.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages