Breaking

Friday 14 October 2022

WIZARA YAAHIDI KUFUFUA MUZIKI WA DANSI, TAMASHA KUBWA KUFANYIKA NOVEMBA MWAKA HUUNa John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inakwenda kufufua muziki wa dansi uliokuwa ambao umeanza kupotea kwa kuratibu tamasha kubwa la muziki wa dansi Novemba mwaka huu.

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akimkaribisha Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Komredi Abdurahaman Kinana kwenye usiku wa Tamasha la Muziki la Grand Gala Dance kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha hayati Mwalimu Nyerere leo Oktoba 14, 2022 jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa kutokana na kuendelea kufifia kwa muziki wa Dansi Wizara inawakaribisha wadau mbalimbali na kushirikiana nao kwa ajili ya kutoa maoni ya jinsi ya kurejesha utamaduni wa muziki huo.

" Kama nilivyoahidi mara baada ya kuteuliwa kusimamia Wizara hii kuwa Milango yangu ya Ofisi ipo wazi, Ninawakaribisha wadau wote wenye maono, mawazo ya jinsi ya kuurejeshea thamani yake muziki wetu wa asili muziki wa dansi, tutashirikiana nanyi wakati wote, tutawasikiliza na kuwaunga mkono kila mwenye wazo ambalo linatuunganisha pamoja na kuturejesha kwenye fikra za Mwalimu." Amesisitiza Mhe, Mchengerwa


Ameongeza kuwa muziki wa dansi una mchango mkubwa kwenye uhuru wa nchi yetu na ukombozi wa bara la Afrika kwa ujumla hivyo kuna umuhimu wa kuufufua.

Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa kutokana na mchango wa Sanaa na Utamaduni, Serikali imeanzisha Mfuko wa Sanaa utakaowasaidia wasanii ili waweze kutumia kuboresha kazi zao.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu na kuzipa kipaumbele sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo (sekta za kimkakati) ambazo kimsingi ndio chimbuko la Utamaduni.Amesema mataifa yote duniani yanatambuliwa na kutofautishwa na utamaduni wa taifa husika na katika karne hii ya Utandawazi mataifa mengi yanajitanabaisha kwa kutumia Muziki wake.

"Kwa kutambua hilo tayari Wizara imeshafanya jitihada za kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na mdundo wake wakiasili utakaotutambulisha duniani kote kama ilivyo kwa mataifa ya Jirani, Afrika ya kusini na kwengineko" Ameeleza Waziri Mchengerwa

Tamasha hilo limeendeshwa na mshereheshaji nguli nchini Masudi Masudi huku mwimbaji maarufu na mtunzi wa wimbo wa Tanzania yetu ndiyo nchi ya furaha, Steven Hiza, Mhe. Nape na bendi mbalimbali kutumbuiza.Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages