Breaking

Monday 3 October 2022

NGOs ZATAKIWA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA SERIKALI



Na WMJJWM Dodoma

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yametakiwa kuonesha ushirikiano na uzalendo katika kuwahudumia wananchi katika miradi mbalimbali wanayotekekeleza.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mwantum Mahiza wakati akifungua Kongamano la NGOs kuelekea Jukwaa la Mwaka la Mashirika hayo linalofanyika jijini Dodoma tarehe 03-04 Oktoba, 2022.




Bi. Mwantumu amesema lengo la Serikali ni kuratibu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yaweze kusaidiana katika kutoa huduma kwa jamii pale Serikali ilipoishia katika maeneo mbalimbali.




Ameongeza kuwa ushirikiano ndio nyenzo muhimu katika kuhakikisha Mashirika hayo na Serikali yanaweka nguvu ya pamoja kutoa huduma kwa jamii kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.




"Naomba tuwe mfano katika kushirikiana na Serikali na tuwe filimbi ya kuishauri na kusaidia Serikali katika mambo ambayo hayaendi sawa ili tuweze kuleta maendeleo katika taifa" alisema Bi. Mwantumu




Aidha ameyaomba Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuhakikisha yanafuata vipaumbele vya Serikali katika kutekeleza afua mbalimbali na miradi yao ili waweze kusaidia Taifa kuleta maendeleo na ustawi wake.




Naye Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) Vickness Mayao amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs imeshirikiana na Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) katika kuratibu Jukwaa la Mwaka la Mashirika hayo ili kuweka mikakati na Mipango madhubuti ya kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanasaidiana na Serikali kuwahudumia wananchi kupitia utekelezaji wa miradi yao.




Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Revocatus Sonna amesema Baraza hilo limeratibu Majukwaa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika ngazi ya Mikoa na Wilaya ambapo yamekuwa na maazimio mbalimbali ambayo yatawasilishwa katika Jukwaa Kuu la Mwaka ili kuwe na muelekeo wa pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao.




Kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuelekea Jukwaa la Mwaka la NGOs linafanyika kwa lengo la kupata mrejesho wa kupata kutoka katika Jukwaa lililopita na Majukwaa yaliyofanyika katika Mikoa na Wilaya kuelekea Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2022.




MWISHO
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages