Breaking

Thursday 20 October 2022

RAIS SAMIA ATAKA SHERIA KUTOA KIPAUMBELE KWA WANAWAKE



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inahitaji Sheria madhubuti kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na umiliki wa rasilimali.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais ikulu Zuhura Yunus imeeleza kuwa Rais Samia amesema hayo leo Alhamisi Oktoba 20, 2022 kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (Women in Law and Development in Africa — WiLDAF) yaliyofanyika ukumbi wa Serena.

Aidha, Rais Samia amesema licha ya takwimu kuonyesha kuwa asilimia kubwa ya wanawake wanajishughulisha na shughuli za uzalishaji, bado baadhi ya mila na desturi zinawafanya wanawake kuendelea kukandamizwa.

Rais Samia pia amesema Sheria ni nyenzo kuu ya ufikiwaji wa usawa wa kijinsia na ustawi wa wanawake hivyo kutoa kipaumbele kwa wanawake ni jambo la lazima ili kuleta maendeleo.

Vile vile, Rais Samia amesema ipo haja ya kufanya tathmini ya Sheria zilizopo na kuona Zina mchango gani kwa Watanzania na kuhakikisha kuwa zinakwenda ngazi za chini ili ziweze kutambuliwa na kufahamika kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa Sheria kutungwa na kutafsiriwa kwa Iugha ya Kiswahili ili kurahisisha kutoa elimu na ufahamu kwa wananchi.

Rais Samia ameiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Wasaidizi wa masuala ya Sheria kuwashirikisha wananchi na viongozi wa dini na kimila katika kuondoa vitendo vya udhalilishaji na ukandamizaji dhidi ya mwanamke.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages