Breaking

Thursday 20 October 2022

WATUMISHI 262,800 WAPANDISHWA MADARAJA



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Jenista Mhagama amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewapandisha madaraja watumishi 262,800 hadi kufikia Septemba 2022.

Ametoa kauli hiyo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipopewa nafasi kuzungumza na viongozi wa mkoa, wilaya na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma kwenye kikao alichokiitisha ili kuwakumbusha watumishi wajibu wao

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hadi kufikia Septemba, 2022 ameshawapandisha madaraja watumishi 262,800 ambao kwa miaka zaidi ya mitano walikuwa hawajapanda. Na kila mwezi Serikali inatumia sh. bilioni 58.3 kulipia mishahara iliyopandishwa,”

“Tarehe 22 Aprili, 2021 Mheshimiwa Rais Samia alilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza na kuweka vision yake. Mheshimiwa Rais anatambua kuwa rasilmali watu ndiyo inasimamia rasilmali fedha. Na ndiyo maana Serikali inagharamia sana uendelezaji wa rasilmali watu nchini.”

Amesema katika bajeti ya mwaka 2022/2023, watumishi 120,210 wametengewa fedha ili wapandishwe madaraja. “Hii ni kutokana na ukweli kuwa tulikuwa na watumishi 67,000 wa mwaka 2015, 2016 na 2017 ambao walikuwa na barua za kupanda madaraja lakini zilifutwa na wala hawakupandishwa madaraja hayo.”

“Naomba niwahakikishie kuwa Mheshimiwa Rais ameagiza kuwa hawa wote wapandishwe madaraja na kabla sijaja ziara hii, nilicheki taarifa za mfumo wa hali ya utumishi na hali ya mshahara na kukuta wote wamepandishwa madaraja ila wanatofautiana kwenye ngazi na miaka ya utumishi. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais ameagiza kuwa wote wapandishwe kwa mserereko,” amesema.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages