Breaking

Monday 31 October 2022

SIMIYU, RUKWA , PWANI WAPIGWA MSASA MPANGO WA UTAYARI (SRP)



OR -TAMISEMI

Washiriki 34 kutoka katika Mkoa wa Simiyu,Rukwa na Pwani wameshiriki mafunzo ya mpango wa utayari unaomwandaa mtoto kuanza shule (SRP) ambayo yatadumu kwa siku tano kuanzia 31 Oktoba hadi 4 Novemba, 2022 Jijini Dodoma.

Washiriki ni Maafisa Elimu Taaluma Wilaya, Waratibu wa Elimu pamoja na walimu mahiri wa elimu ya awali kutoka katika Halmashauri 15 za Mikoa ya Pwani, Rukwa na Simiyu.

Mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo ya awali waliopewa washiriki hao ili kuwajengea uwezo Wasaidizi Jamii wa Walimu wanaowafundisha watoto ambao hawajapata fursa ya kujiunga na Elimu ya awali kutokana na changamoto mbalimbali.

Mafunzo yamelenga kumjengea mtoto umahiri katika utambuzi pamoja na matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mawasiliano huku hadithi, michezo pamoja na nyimbo zikitumika kama nyenzo za kufundishia.

Watoto watapatiwa mafunzo kwa muda usiongupungua wiki kumi na mbili ambapo hadi kufikia sasa tayari mafunzo haya yameshafanyika kwa wiki nne.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa shule bora kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Winfrid Chilumba amesema kuwa mbali na muendelezo wa mafunzo haya, washiriki watatumia fursa hii kutoa mrejesho wa mafunzo ya utayari yaliyokwisha fanyika kwa watoto hao kwa wiki nne.

Naye Mwanaisha Abdul Omary mshiriki kutoka katika Halmashauri ya Mji Bariadi amesema mafunzo haya yana tija katika jamii kwakuwa yanampa mtoto fursa ya kupata elimu ya awali na kumuandaa kwa ajili ya Elimu ya Msingi hasa kwa watoto ambao wanaishi mbali na shule.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages