Breaking

Tuesday 29 November 2022

DKT. BITEKO ATOA MAAGIZO KIWANDA CHA MBEYA CEMENT


Kiwanda cha uzalishaji Saruji cha Mbeya Cement Company Limited (MCC) kimeelekezwa kuandaa Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na kuuwasilisha katika Halmashauri husika ili upitiwe kwa lengo la kupata kibali kwa ajili ya utekelezaji.

Maelekezo hayo, yametolewa na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko baada ya kutembelea Kiwanda hicho kilichopo jijini Mbeya kwa lengo la kukagua shughuli zinazoendeshwa kiwandani hapo.

Dkt. Biteko amesema, Sheria ya Madini Sura 123 inazitaka Kampuni za uchimbaji madini nchini kuajiri wataalamu wa ndani na kutumia bidhaa na huduma kwa kadri zinavyopatikana nchini na kwa zile zinazohitaji kutoka nje, Kampuni za uagizaji sharti ziwe na Watanzania wenye umiliki wa hisa zisizopungua asilimia 20.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema shughuli za uchimbaji zinazoendelea katika eneo hilo, ipo haja ya kuziboresha ili wakati wa ufungaji wa mgodi zisilete shida katika utekelezaji wake.

"Tumekuja kukagua namna wanavyochimba na tumebaini kuwa, upo uchimbaji ambao lazima waboreshe ili wakati wa ufungaji wa mgodi isiwe shida kwa sababu namna wanavyochimba wakati mwingine wanakiuka taratibu ndogo ndogo za kiuchimbaji ambazo timu yetu ya wataalamu itawaelekeza," amesema Dkt Biteko.

Aidha, Dkt Biteko ameipongeza Kampuni hiyo kwa kutumia wataalamu wa ndani na huduma zinazopatikana nchini ambapo zaidi ya asilimia 90 kampuni hiyo imetekeleza takwa hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mbeya Cement Company Limited Khaled Ghareib amemshukuru Dkt. Biteko kwa kutembelea Kiwanda hicho ambapo ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Wazazi wa Madini.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya Oscar Kalowa amesema MCC inatoa ushirikiano mzuri kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho na inachangia maduhuli ya Serikali kwa wakati na kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages