Breaking

Friday 18 November 2022

MILIONI 300 KUJENGA KITUO CHA AFYA SAME



Na Mwandishi Wetu, Same

SERIKALI imetoa Sh.milioni 300, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha kata ya Vunta wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk.Festo Dugange wakati wa ziara aliyofanya katika Jimbo la Same Mashariki kukagua miradi ya maendeleo.

Alisema Kituo cha Afya Vunta kilichopo kimechakaa, hivyo ni imani yake fedha hizo ambazo zimetolewa na Serikali zitatumika vizuri kujenga upya, ili wananchi waweze kupata huduma bora.

“Majengo yaliyopo yamechaa sana, tumesikia kilio chenu kupitia Mbunge wenu Anne Kilango, Rais Samia Suluhu Hassan ameruhusu Sh.milioni 300 zitolewe kwa ajili ya Vunta naamini mtapata huduma bora kikikamilika,” alisema.

Dk Dugange alitoa maelekezo kwa viongozi wanaohusika kuhakikisha ujenzi huo unaanza mara moja, huku akisisitiza ujenzi huo uzingatie uwepo wa majengo ya upasuaji na chumba cha kuifadhia maiti, ili wananchi wasipate tabu kutembea zaidi ya kilometers 25 kufata huduma ya afya.

Naibu Waziri Dugande alimwagia sifa Mbunge Kilango kwa kuchapa kazi na kuwapigania wapiga kura wakeakiwa bungeni, ili waweze kupata huduma za kijamii bora na nzuri.

Alisema ameridhishwa na miradi ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Mihamba, zahanati inayogharimu Sh.milioni 500 na barabara ambazo zitapunguza adha ya usafiri katika vijiji vya Same Mashariki.

Naye Mbunge Kilango alisema anatoa shukran kwa Rais Samia kwa kuwapatia fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Vunta ambacho amekuwa akikiombea fedha bungeni mara kwa mara.

Kilango alisema lengo lake ni kuona wananchi wake hawapati tabu kwenye mahitaji muhimu kama afya, elimu, maji na barabara , ili waweze kupitisha mazao yao kwa wepesi zaidi na kuwapatia wananchi miradi tofauti wajikwamue kiuchumi

Mwisho

.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages