Breaking

Wednesday 16 November 2022

WAAJIRI WAONYWA KUFICHA BARUA ZA UHAMISHO WA WATUMISHI WA UMMA



Na. Veronica Mwafisi, Kigoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amekemea tabia ya baadhi ya waajiri katika Taasisi za Umma kuficha barua za uhamisho wa watumishi wa umma ambao Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ameridhia na kutoa kibali cha uhamisho ili wakautumikie umma katika maeneo mengine ya nchi ambayo mamlaka imeona kuna uhitaji.

Akizungumza Novemba 15, 2022 na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ndejembi amesema, waajiri na Maafisa Utumishi wanapaswa kutenda haki kwa watumishi wa umma ambao wanastahili kuhama baada ya kupatiwa kibali cha uhamisho na mwenye mamlaka ambaye ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, na si kufichiwa barua zao za uhamisho kwa lengo la kukwamisha mchakato wa uhamisho.

“Waajiri na Maafisa Utumishi tendeni haki kwa watumishi wa umma ambao wanastahili kuhama baada ya uhamisho wao kuridhiwa na mamlaka, tusifiche barua zao kwani kitendo hicho kinakwenda kinyume na mamlaka na ni kinyume cha Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, wapo watumishi wa umma ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi, hivyo mamlaka kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu-UTUMISHI ikaamua kumpeleka mtumishi huyo katika eneo lingine la kazi ili abadili mazingira ya kazi ambayo yatamuongezea ufanisi kiutendaji, lakini baadhi ya waajiri hukwamisha uhamisho huo wakati mamlaka iliridhia baada ya kufanya uchambuzi yakinifu.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka waajiri katika Taasisi za Umma kutopitisha barua za kuomba uhamisho za watumishi ambao ni ajira mpya, kwani ajira zao hazina muda mrefu na baadhi yao wanakuwa hawajathibitishwa kazini, hivyo kutotimiza kigezo cha kutumikia miaka mitatu tangu waajiriwe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ester Mahawe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi walio katika wilaya yake.

Mhe. Mahawe, amewahimiza watumishi wa umma walio katika eneo lake la utawala, kufanya kazi kwa bidii na weledi kama alivyoelekeza Mhe. Ndejembi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kwa vitendo Kaulimbiu ya KAZI IENDELEE ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Naye, Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Ujiji, ambaye ni Afisa Utumishi, Bw. Stafordi Bidebuye amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kwa kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa Halmashauri hiyo kwa muda mrefu.

Mhe. Bidebuye amesema kupitia elimu ya masuala ya kiutumishi waliyoipata kutoka kwa Mhe. Ndejembi, anaamini Mkoa wa Kigoma utafunguka katika kila sekta na kupata maendeleo chini ya uongozi makini wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameanza ziara ya kikazi mkoani Kigoma yenye lengo kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).









Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages