Breaking

Sunday, 13 November 2022

WADAU WAHIMIZWA KURASIMISHA BIASHARA ZAO



Wafanyabiashara nchini wamehimizwa kurasimisha biashara zao ili waweze kupata firsa mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kibenki.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 13 Novemba, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo, Bw. Ibrahim Mwangalaba, alipotembelea Banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwenye maonesho ya kwanza ya Biashara yanayofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), Usharika wa Temboni, Jijini Dar es Salaam.


Bw. Mwangalaba amesema BRELA ni kiungo muhimu kwa wafanyabiashara kwani huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi za kibenki kwa wafanyabiashara, BRELA hushirikishwa ili kupata taarifa za wafanyabiashara husika.

"Tumieni fursa hii kurasimisha biashara zenu ili mpate fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ikiwa ni pamoja na mikopo," amesisitiza Bw. Mwangalaba.


Bw. Mwangalaba pia ameipongeza BRELA kwa kutoa huduma za papo kwa papo za Usajili wa Majina ya Biashara, kampuni na utoaji wa leseni za Biashara Kundi 'A' kwa wadau wanaokamilisha taratibu za urasimishaji.

"Ninawapongeza kwa utendaji wenu wa kazi, kwani mnatekeleza majukumu yenu kwa vitendo, mbali na kutoa elimu kwa wadau kuhusu huduma mnazozitoa," amesisitiza Bw. Mwangalaba.


Ameeleza kuwa Benki ya Maendeleo itaendelea kushirikiana na BRELA katika warsha na makongamano mbalimbali ili elimu ya urasimishaji wa Biashara iweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wadau waliyo tembelea Banda la BRELA kuwa chachu ya mabadiliko kwa wadau ambao hawajapata elimu hiyo.

Katika Maonesho hayo ya siku mbili yanayohitimishwa tarehe 13 Novemba, 2022 yameandaliwa na Benki ya maendeleo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages