Breaking

Sunday 20 November 2022

WAKURUGENZI HALMASHAURI WATAKIWA KUFUATA UTARATIBU UJENZI MIRADI YA ELIMU



Na Angela Msimbira, TABORA

WAKURUGENZI wa Halmashauri nchini wametakiwa kutekeleza miradi ya sekta ya elimu kwa kufuata miongozo ili kupunguza hasara zinazoweza kujitokeza pindi miradi hiyo ikitekelezwa kinyume na utaratibu.

Hayo yameagizwa Novemba 19, 2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki wakati wa kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora mkoani Tabora.

Amesema ni vyema wakurugenzi wakahakikisha wanafuata maelekezo yanayotolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI juu ya ujenzi wa miundombinu ya elimu na kuwa tofauti na hapo wanatakiwa kuomba muongozo wa mabadiliko kabla ya kuendelea na mabadiliko.

“Endapo mna maoni tofauti na maelekezo na miongozo iliyotolewa kabla hujabadilisha au kufanya utekelezaji tofauti ofisi iko wazi tuzungumze.”amesisitiza Waziri Kairuki

Amesema kuna Halmashauri ambazo zimeanza kutekeleza wanavyoona wao, sidhani kama itajitokeza hapa Tabora, una maoni tofauti wasilisha maoni kabla hujafanya tofauti, kila mtu akijiamulia anaenda anavyotaka hatutakuwa na utaratibu.

Aidha, Waziri Kairuki amesisitiza ushirikishwaji wa jamii na viongozi katika kuibua miradi inayopaswa kutekelezwa katika Halmashauri husika ili fedha zipelekwe eneo lenye uhitaji.

“ Tujitahidi kuwashirikisha maafisa elimu, madiwani wetu, wabunge pamoja na wananchi wengine ili kupata orodha sahihi, ili tukifanya maandalizi yetu ya kuleta fedha za ujenzi wa shule za msingi au kama ni ukarabati basi tunauhakika tunazileta kwenye maeneo yenye uhitaji, tusipofanya hivyo itakuwa ni mtihani.” amesema

(mwisho)
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages