Breaking

Tuesday 8 November 2022

WATAALAMU KUTOKA UFARANSA KUWASILI NCHINI KUFANYA UCHUNGUZI AJALI YA NDEGE




Wataalam kutoka Kampuni ya ATR nchini Ufaransa ambao ndio watengenezaji wa ndege ya Precision Air iliyopata ajali wanatarajiwa kuwasili ili kuungana na timu ya wataalam waliopo.

Kauli hiyo imetolewa Novemba 08, 2022 na msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akitoa ufafanuzi wa baadhi ya taarifa kutoka serikalini juu ya kinachoendelea baada ya ajali ya Ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6 mwaka huu Mkoani Kagera.

Amesema Kitengo maalum cha uchunguzi wa ajali za anga kimeanza kazi yake tangu ajali ilipotokea, mpaka sasa na kuwa kifaa cha mawasiliano kwa ajili ya kuwezesha uchunguzi kufanyika kimeshapatikana na taratibu za uchunguzi zinaendelea.

Msigwa amesema kuwa timu ya watengenezaji wa injini pia watafika kwa ajili ya uchunguzi wa ajali hiyo.

Aidha ameongeza kuwa ajali ni kitu ambacho hakina macho kinaweza kutokea wakati wowote, huku akiwahakikishia Watanzania kuwa Serikali inaendelea kufanya juhudi kuhakikisha inaimarisha usalama katika usafiri wa anga katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, usafiri wa anga ni salama kuliko usafiri wowote.

"Serikali itaanza mara moja kununua vifaa na kuvipeleka maeneo mbalimbali ambapo majanga yanaweza kutokea, tutafundisha wataalam na jamii juu ya namna bora ya kukabiliana na majanga"alisema Msemaji mkuu.

"Tunatarajia kuanza programu kubwa ya kutoa mafunzo kwa vijana na wadau juu ya namna ya kukabiliana na majanga na tunaendelea kuimarisha ofisi zetu za Zimamoto na Uokoaji ambapo katika bajeti ya mwaka 2022/23, zimetengwa Shilingi bilioni 9.9 kwa ajili ya kuboresha huduma katika eneo hilo"
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages