Breaking

Saturday 5 November 2022

WATUMISHI GST WAPATA MAFUNZO YA KUZINGATIA MAADILI NA UADILIFU WA UTUMISHI WA UMMA



Na.Samwel Mtuwa- DODOMA

Watumishi zaidi ya 150 wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini wa Tanzania ( GST) wamepata Mafunzo juu ya kufanya kazi kwa kuzingatia Maadili na uadilifu wa Utumishi wa Umma katika semina ya Maadili na Mapambano dhidi ya Rushwa mahali pa kazi iliyofanyika leo novemba 5, 2022 mkoani Dodoma.

Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba aliwaambia Watumishi wote walioudhuria semina hiyo kufuatilia na kusikiliza kwa makini mada zitakazowasilishwa na watoa mada kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania ( TAKUKURU) kwasababu mada hizo zitamsaidia mtumishi kufanya kazi kwa kufuata misingi ya Utumishi wa Umma kama inavyoelekeza na kuboresha Mazingira yetu ya kazi.



Dkt.Budeba alisisitiza kuwa tunahitaji jamii yenye ustawi na kuwa na Maadili Katika kutekeleza majukumu yetu ili kufikia malengo tuliyopewa na serikali na kuifikia GST mpya.

Mtaalam kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Getruda Chiunga akitoa mada kuhusu uzingatiaji wa Maadili katika Utumishi wa umma alieleza kuwa ili mtumishi wa umma awe mwenye ufanisi na kuheshimika anapaswa kuzifuata kanuni za maadili ya utumishi pamoja na kuwa na tabia na mienendo mizuri katika kutimiza majukumu yake.


Alitaja baadhi ya mienendo hiyo kuwa ni kuzifuata kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma Kwa kutoa Huduma Bora, Utii Kwa Serikali, Bidii ya kazi , kutoa Huduma bila upendeleo , Kufanyakazi kwa uadilifu , kuheshimu sheria na matumizi sahihi ya taarifa za serikali.

" Endapo mtumishi wa umma atafanyakazi kwa kuzingatia mienendo niliyoitaja na kufafanua basi wewe mtumishi utafanya mahali pa kazi kuwa salama" alisema Chiunga


Kwa upande wake Faustine Malecha mtoa mada kutoka TAKUKURU aliwakumbusha Watumishi kuepukana na vishawishi na mitego ya rushwa kwani kutoa au kupokea Rushwa ni kosa la kisheria ambapo adhabu yake kutiwa hatiani au kufungwa.

Mbali ya hapo Malecha aliwasii Watumishi kuwa makini na zawadi zinazolewa mahali pa kazi kwasababu vifungu vya kisheria vinatambua kuwa zawadi ni sehemu ya kishawishi kwa mtumishi.




Mapema baada ya kukamilika kwa semina hiyo watumishi wote walikula kiapo kwa kusoma Ahadi ya Uadilifu kwa Utumishi wa Umma ili kutambua dhamira ya kuufanya utumishi wa umma kuwa wenye ufanisi na kuheshimika kwa kufuata Sheria namba 8 ya Mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003 na 2005.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages