Breaking

Wednesday 9 November 2022

WAZIRI BITEKO AWATAKA MAAFISA MADINI KUTUNZA TAKWIMU, KUFANYA KAZI KWA WELEDI




Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa nchini kuhakikisha wanatunza takwimu za madini ya aina zote yanayozalishwa nchini katika kanzidata sambamba na kuendelea kusimamia vyema Sekta ya Madini ili mchango wake kwenye Pato la Taifa uendelee kukua na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Waziri Dkt. Biteko ametoa agizo hilo leo Jumatano Novemba 09, 2022 kwenye kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kukula, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, wakurugenzi, mameneja na maafisa madini wakazi wa mikoa nchini.

“Pamoja na kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kusimamia Sekta ya Madini katika mikoa yenu, ninawataka kuendelea kuchapa kazi katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa na serikali ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa maduhuli na ukuaji wa mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa yanafikiwa pamoja na kuhakikisha taarifa za uzalishaji wa madini ya aina zote zinakuwepo kwenye kanzidata ili kupata picha halisi ya mwenendo wa ukuaji wa Sekta ya Madini nchini,” amesisitiza Biteko

Aidha, amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 na kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli lililowekwa na Serikali kwa mwaka 2022-2023 la shilingi bilioni 822 sambamba na uboreshaji wa huduma kwa wadau wa madini.

Amesisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kuipa ushirikiano Tume ya Madini ili kufikia malengo yake ikiwa ni pamoja na kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba Sekta ya Madini.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuendelea kufanya kazi kwa weledi ikiwa ni pamoja na kutoa leseni za madini kwa haki na kupambana na vitendo vya rushwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages