Breaking

Wednesday 9 November 2022

TANZANIA, NORWAY KUIMARISHA USHIRIKIANO KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo leo tarehe 9 Novemba 2022 katika vikao vya pembezoni mwa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi jijini Sharm El Sheikh nchini Misri, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Bi Anne Veathe Tvinnereim katika banda la maonesho la Tanzania.

Katika mazungumzo hayo, mawaziri hao wamejadili na kukubaliana kuendeleza ushirikiano katika masuala ya maendeleo na hususan ufadhili katika miradi ya hifadhi ya mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo amesema Serikali ya Tanzania na Norway zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika sekta mbalimbali na kusisitiza kuwa kwa sasa masuala ya mazingira yanazidi kupewa kipaumbe katika ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo ya Kimataifa wa Norway Bi. Anne Veathe Tvinnereim amesisitiza kuwa nchi ya Norway itaendelea kushirikiana na kufadhili miradi ya mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania kwa lengo la kusaidia wananchi walio katika hatari kubwa ya kuathiriwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Waziri Jafo alimshukuru Bi Anne Veathe Tvinnereim na Serikali ya Norway kwa ujumla kwa ushirikiano na misaada katika sekta mbalimbali za kiuchumi kwa Tanzania. Alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na Serikali ya Norway na kuendeleza ushirikiano huo kwa maslahi mapana ya nchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Alisisitiza kuwa ajenda ya mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa duniani na inahitaji ushirikiano na ufadhili wa nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages