Breaking

Saturday, 3 May 2025

TBS- Mafuta Yaliyosababisha Madhara Yombo Dovya Yaliingia Nchini Yakiwa Salama


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

 SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limebaini mafuta ya kupikia yaliyosababisha athari kwa  wakazi wa eneo la Yombo Dovya, Jijini Dar es salaam, yalikuwa yameharibika na ndani yake kubeba aina mbili za kemikali ambazo kitaalamu ni (E,E)2,4-Decadienal na decena. Kemikali hii hutokana na mafuta hayo kupikwa katika joto kali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 02,2025, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga amesema ufuatiliaji ulifanyika na kugundua kuwa mafuta hayo yaliagizwa  kwa kupitia njia halali za uingizaji wa bidhaa nchini, kutoka nchi ya Indonesia kupitia muagizaji mkubwa ambaye ni LONG WIDE TRADERS LTD  yakiwa Yako salama.

"Muagizaji huyu, kati ya Novemba na Disemba 2024 aliingiza mafuta madumu 7500 hapa nchini, ambapo kila dumu lina ujazo wa lita 20 kwa ujumla ni sawa na lita 150000, hivyo basi kama mafuta hayo yangekuwa na shida basi madhara yangekuwa makubwa zaidi". Amesema.

Aidha amesema baada ya kufuatilia namna mafuta yalivyoingia nchini na kugundua hakuna dosari, walifuatilia mnyororo wa mauzo ambapo muuzaji wa jumla, Ally Fadhil Ally alipokea sehemu ya mafuta hayo, ambapo alianza kuuza, na katika kipindi hicho likatokea tukio la madhara ya mafuta hayo, alikuwa amebakiwa na madumu 99.

"Wakati tunafatilia baada ya mlipuko  tuligundua madumu  hayo 99 yalikuwa na kasoro, hayakuwa yamefungwa na lakiri halisi ya mtengenezaji "Amesema Bw. Msasalaga

Aidha, ilielezwa kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa muuzaji huyo wa duka la jumla kutokana na kukiuka taratibu za uhifadhi wa mafuta hayo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages