Breaking

Saturday 31 December 2022

CRISTIANO RONALDO ATIMKIA UARABUNI



Na Ayoub Julius

Klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia imethibitisha kumsajili Gwiji wa soka raia wa Ureno Cristiano Ronaldo katika klabu hiyo.

Habari za kusajiliwa kwake zilithibitishwa Ijumaa jioni na akaunti rasmi ya Twitter ya klabu hiyo, iliyoandika kwenye mtandao wa Twitter

"Mwanasoka mkubwa zaidi duniani asainiwa rasmi" sambamba na picha za Ronaldo akiwa ameinuka juu shati ya Al Nassr.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 aliondoka Manchester United baada ya kusitishwa kwa kandarasi yake mwezi Novemba na amekuwa mchezaji huru tangu wakati huo baada ya kutofautiana na klabu hiyo kutokana na kushindwa kuhama msimu wa joto na mahojiano aliyoyafanya na Mtangazaji maarufu Piers Morgan na kuzua taharuki kati yake na waajili wake.

Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or ametia saini kandarasi hadi mwaka 2025, tetesi za hapo awali zilisema kwamba Ronaldo atakuwa akilipwa pauni milioni £250 iwapo angesaini katika klabu hiyo.

Ripoti zimesema Ronaldo amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu na atalipwa pauni milioni 62 (€69.9m) kwa msimu.

Uhamisho wa Ronaldo unaonekana kuonyesha zaidi ukubwa katika historia ya Soka la Ulaya.

Ronaldo amenyakua taji la Ligi ya Mabingwa mara tano, mara nne akiwa na Real Madrid na mara moja akiwa na United, huku idadi yake ya mabao 140 ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika michuano hiyo mikuu ya vilabu barani Ulaya.

Ronaldo pia ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Madrid akiwa na mabao 450, huku akiwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya soka la kimataifa la wanaume mwaka jana sasa akiwa na mabao 118 kwa Ureno.

Al Nassr wananolewa na kocha wa zamani wa Lyon, Rudi Garcia na huku wakiwa na mshambuliaji wa Cameroon Vincent Aboubakar na kipa wa zamani wa Arsenal David Ospina miongoni mwa kikosi chao.

Timu hiyo yenye maskani yake Riyadh imeshinda ligi kuu ya Saudi Arabia kwa mara tisa idadi ambayo imezidiwa na Al Hilal ambao wana mataji 18.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages