Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amewataka wawezeshaji stadi za maisha kuhakikisha elimu hiyo inawafikia vijana wasio na Ulemavu na wenye Ulemavu ili waweze kutambua uwezo wao wa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za ujenzi wa Taifa.
Naibu Waziri Katambi ametoa maagizo hayo wakati akifunga mafunzo ya stadi za maisha (Life Skills) kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu katika ukumbi wa Midland hoteli, mkoani Mwanza huku akieleza lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa elimu ya stadi za maisha inajumuishwa kwenye afua na programu za kushughulikia changamoto za vijana ikiwemo vijana wenye Ulemavu
Amesema kuwa, elimu ya stadi za maisha ni muhimu kwa kuwa inawajenga vijana na kuwapatia mbinu na maarifa ambayo yatawasaidia kutambua fursa zilizopo, namna ya kuweza kuzifikia na kujikwamua kiuchumi.
“Vijana wakipatiwa elimu ya stadi za maisha watahamasika kuwa na mabadiliko chanya ya tabia, mienendo na mitazamo. Natumaini mtatumia elimu hii kuhakikisha kwamba kunakuwa na mafunzo ambayo yatawasaidia vijana kuwa na mbinu na maarifa mbalimbali zitakazo wawezesha kujitambua, kuwa na uthubutu na kufanya maamuzi sahihi,”
Ameongeza kuwa, ifikapo mwaka 2023 idadi ya waelimishaji wa stadi za maisha kitaifa inatarajiwa kufika 352 kutoka idadi ya wawezeshaji 142 waliopo kwa takwimu za mwaka 2022, ongezeko hilo itakuwa sawa na 60.2% ya lengo lililokusudiwa, hivyo kutakuwa na ongezeko kubwa la idadi ya waelimishaji rika wanaotarajiwa kutoa elimu ya stadi za Maisha kwa vijana wengi zaidi.
Aidha, Naibu Waziri katambi amesema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kushughulikia masuala mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeendelea kusimamia na kutekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi mbalimbali ikiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika kuimarisha ustawi wa Watu wenye Ulemavu nchini, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya stadi za maisha kwa vijana wenye Ulemavu ili waweze kujitambua, kuwa na uthubutu, kufanya maamuzi sahihi na kuepuka vishawishi pamoja na mazingira hatarishi.
Sambamba na hayo ameeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha Vyuo vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu sita ikiwemo Yombo – Dar es Salaam, Luanzari - Tabora, Mtapika - Mtwara, Sabasaba - Singida, Mirongo – Mwanza na Masiwani – Tanga. Sambamba na ujenzi wa vyuo vipya 3 katika mkoa wa Songwe, Ruvuma na Kigoma.
“Ni wajibu wetu kuwatambua Watu wenye Ulemavu, kuwasikiliza na kuwahudumia,” amesema
Pia, ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuwezesha kutoa mafunzo hayo ya stadi za maisha (Life Skills) kwa wakufunzi na watendaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu.