Breaking

Tuesday 6 December 2022

TANZANIA, COMORO KUIMARISHA USHIRIKIANO SEKTA YA AFYA



Na WAF – Dar Es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi leo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Comoro nchini Tanzania Dkt. Ahamada El Badaoui kujadili namna ambavyo nchini hizo zinaweza kushirikiana katika maendeleo ya Sekta ya Afya.


Katika mazungumzo yao viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana kuboresha uhusiano wa kutoa tiba kwa wagonjwa wanaotoka Comoro na kuja kupata matibabu ya Kibingwa katika Hospitali za Taifa na kanda.


Prof. Makubi amesema Serikali ya Comoro imepanga kufanya maonesho ya kimataifa ya sekta ya afya ambayo yatashirikisha Tanzania na nchi nyingine yatayayofanyika januari mwakani na kwamba hiyo itakua fursa kwa watoa huduma za afya ikiwemo hospitali na kampuni za dawa na wananchi kwa ujumla kujumuika kwa pamoja katika maonesho ili kutangaza shughuli zinazofanywa na sekta ya afya nchini.


“Hii ni fursa nzuri nawaomba watanzania wajiandae ili kuweza kuonesha ni huduma zipi tunatoa na azma yetu kama Serikali kuifanya Tanzania iwe chombo cha kutoa utaalamu na vilevile kutoa huduma kwa maana ya Medical Tourism, tunataka kuhakikisha kwamba vituo vyetu vinakua na huduma iliyobora ambayo itavutia wagonjwa kutoka nchi zingine” amesema Prof. Makubi


Aidha amesema taasisi za serikali na sekta binafsi zitaendelea kushirikiana na Comoro kwa kuwapatia mafunzo wataalamu mbalimbali ambao wanapenda kuja kusomea hapa nchini.


Kwa upande wake Balozi wa Comoro nchini Dkt. Ahamada El Badaoui ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali kuendelea kushirikiana na nchi hiyo na kueleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Comoro ni wa muda mrefu na wenye manufaa.


Amefafanua kuwa Comoro imekua pia ikishirikiana na hata Hospitali binafsi zilizopo nchini na yote hiyo imetokana na kuwa na mahusiano mazuri baina ya pande zote mbili.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages