Breaking

Sunday 18 December 2022

WAZIRI MASAUNI AMALIZA MGOGORO WA ARDHI GEREZA KING’ANG’A NA WANANCHI ULIODUMU KWA MIAKA 44




Na Felix Mwagara, MoHA, Kondoa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amemaliza mgogoro wa ardhi ulioanza mwaka 1978 kati ya Gereza la Mifugo la King’ang’a na Wananchi wa Vijiji vya Kata ya Kingale, Wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma.

Waziri Masauni akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wataalamu wa ardhi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi pamoja na Maafisa Magereza, waliwasili katika Gereza hilo lililopo katika Mtaa wa Chemchem, leo Disemba 18, 2022 na kufanya kikao cha ndani kwa zaidi ya saa mbili.

Baada ya kikao hicho, kabla ya Waziri Masauni kuzungumza na wananchi wa Kata hiyo, akiwa na viongozi wenzake, walitembelea na kufanya ukaguzi wa eneo la mgogoro na kuona eneo linalogombewa na pande zote mbili kwa miaka yote hiyo.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Iyori, katika Kata hiyo, Waziri Masauni alianza kwa kutoa pole kwa wananchi hao kutokana na mgogoro huo uliodumu kwa miaka mingi na kuwaambia kuwa mgogoro huu umefikia mwisho na ile kauli ya kusema kuwa jambo hili limeshindikana miaka nenda rudi, kuanza sasa itakua historia iliyopitwa na wakati.

“Kabla ya kufika hapa tulikua na kikao, tumekaa, tumejadili kwa kina, na mimi ndio nimepewa dhamana hii ya kulisimamia Jeshi la Magereza kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, na kwa maelekezo ambayo nimepewa na Mheshimiwa Rais kuhusu utatuzi na uondoaji wa changamoto za wananchi ikiwemo hapa Kondoa, tumepeana muda wa wiki mbili, tarehe 30 mezi huu Serikali inataka kulifunga rasmi jambo hili liweze kuisha kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi mliopo hapa ambao mnatumia ardhi ile kwa kilimo, muweze kupata ardhi ya kuendeleza shughuli zenu za kilimo bila bugudha bila usumbufu wowote,” alisema Masauni, na kuongeza kuwa;

“Pia tumekubaliana katika kipindi cha siku hizi za wiki, mbili kwa kupitia watalaamu wetu, tukae tufanye tathimini ya kina uhitaji wa matumizi kati yenu nyinyi na Magereza ili tuweze kutoa mgao utakaokidhi pande zote mbili, naombeni sana mapendekezo na maamuzi hayo yatakapotoka muweze kuyaunga mkono kwasababu yatakua yamezingatia sana maslahi yenu wananchi wa Wilaya ya Kondoa.”

Alisema baada ya maamuzi hayo kuanzia sasa wananchi hao wataendelea kufanya shughuli zao za kilimo na watatumia fursa nyingi mbazo Serikali ya awamu ya Sita ikiwemo kuiongezea Bajeti kwa kiwango kikubwa ya sekta ya kilimo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema mgogoro huo ameukuta ofisi kwake, ni wa muda mrefu na mara kadhaa umeshughulikiwa pasipo na ufumbuzi, hivyo kwa ujio wa Waziri Masauni mgogoro huo utamalizwa.

“Mheshimiwa Waziri jambo alilokuwa amelisema Mheshimiwa Mbunge ni la muda mrefu, kwa namna moja au nyingine makundi mbalimbali yamekuwa yakishughulikia hayakufanikiwa hwakufika mwisho, jambo hili linawahusisha Magereza na wapo hapa,” alisema Senyamule.

Naye Mwakilishi wa Kamishna Jenerali wa Magereza, Kaimu Kamishna wa Magereza Huduma za Urekebu, SACP Omary Salum, alisema jambo hilo nao linawakwamisha, nao hawapendi mgogoro huo uendelee, wanapenda kwenda mbele, lakini muda wowote jambo hilo linakwisha kwa hekima na busara aliyokuwa nayo Waziri Masauni jambo hili litakamilika.

Awali, wananchi walitoa malalamiko yao na mateso waliyopitia katika kipindi cha miaka yote hiyo na kumweleza Waziri huyo wamechoka na wanataka ufumbuzi wa mgogoro huo ambao wanaodai Magereza imechukua ardhi yao.

“Magereza wamevuka mpaka kisheria na kuvamia eneo letu na licha ya viongozi tofauti tofauti kujaribu kutafuta suluhu ya mgogoro huo bila ya mafanikio yoyote, na kupelekea wanakijiji kukosa mahali pakulima na kulisha mifugo,” alisema Mwanakijiji Shaban Mohamedi.

Gereza la King’ang’a lilianzishwa Mwaka Februari 25, 1975 kama shamba la Magereza la mifugo baada ya kupata ardhi kutoka katika Kitongoji cha Chemchem, na upimaji wa awali wa eneo kwa minajili ya kuanzisha mipaka ya Gereza ulianza Juni 25, 1978 na kumalizika Oktoba 1978.

MWISHO
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages