Breaking

Friday 20 January 2023

WAZIRI KAIRUKI ATOA SIKU 14 KWA TUME YA UTUMISHI WA WALIMU



Na Angela Msimbira, MWANZA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki ametoa siku 14 kwa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuwasilisha wizarani orodha ya taarifa sahihi na za kina za walimu wote nchini.

Taarifa zinazotakiwa kuwasilisha ni zile zinazoeleza kwa kina kila mwalimu amejiriwa lini, na nafasi aliyoajiriwa nayo, nafasi au cheo alichonacho kwa sasa, lini amepandishwa cheo na kama hakupandishwa kwa nini na kama mwalimu alijiendeleza na alijiendeleza katika ngazi ipi na eneo lipi.

Kairuki ametoa agizo hilo, Januari 19, 2023, jijini Mwanza wakati wa kufungua kikao kazi Cha mapitio ya tathimini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usambazaji wa elimu nchini.

Amesema TSC inapaswa kuandaa TANGE za Utumishi wa Walimu na kuziwasilisha Ofisi ya Rais –TAMISEMI ndani ya wiki mbili kuanzia sasa lengo likiwa ni kutatua changamoto za walimu.

" Tume hakikisheni mnaandaa TANGE itakayobainisha, mwalimu aliajiriwa lini, nafasi aliyopo, cheo alichonacho kwa sasa, alipanda lini cheo, kwa nini hakupanda cheo, lini alijiendeleza ili Ofisi ya Rais -TAMISEMI ishirikiane na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora kutatua changamoto za walimu nchini."

Amesema kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kujua taarifa sahihi za mwalimu, taarifa za kielimu,uzoefu kazini, taarifa za ajira yake, cheo alichonacho sasa na mwaka aliopandishwa cheo lengo likiwa ni kubaini changamoto za upandaji wa madaraja kwa walimu nchi nzima.

Aidha, Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kuwaonya Wakurugenzi na maafisa utumishi wanaopoka haki za mtumishi wakiwepo walimu bila sababu.

" Badala ya kutumia lugha ya kudhalilisha, kuwanyanyasa na kuwafanyia vitendo visivyofaa, basi mnachopaswa kufanya ni kuwaelimisha watumishi ili wajue kanuni za utumishi wa umma na nyaraka mbalimbali za utumishi."
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages