Breaking

Thursday 19 January 2023

ALIYETUHUMIWA KUMUUA MFANYAKAZI WA TANESCO NAYE AUAWA



Polisi Mkoa wa Songwe imesema mtu anayedaiwa kumuua kikatili mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Angela Shekinyau (33) usiku wa kuamkia Jumatatu ya wiki hii naye ameuawa wakati akijaribu kukimbia akiwa chini ya ulinzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Januari 18, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa Theopista Mallya amesema polisi walimkamata mtuhumiwa Isaya Juma Mazuge maarufu kwa jina la ‘Wa Uyole’.

Kamanda huyo amesema baada ya kukamatwa alitoa ushirikiano kwa kuonyesha vitu vya marehemu Angela ikiwamo simu ya Iphone 11PRO MAX na kuwataja wenzake.

Ameendelea kusema kuwa, mtuhumiwa huyo pia alikuwa na Bastola iliyotengenezwa kienyeji na kwamba waliikuta ikiwa na ganda la shotgun pamoja na mapanga.

Amesema mtuhumiwa alikuwa ameficha silaha hizo kwenye Msitu wa Vwawa Day na baada ya kuonyesha ushirikiano aligeuka ghafla na kuanza kukimbia jambo lililowafanya polisi warushe risasi mbili juu na moja ilifyatuliwa kwake na hatimaye kumpiga na kusababisha kifo.
Kamanda amesema kijana huyo alifariki dunia baada ya damu nyingi kuvuja akipelekwa hospitalini.

Amesema wanaendelea kuwasaka waliotajwa ili wafikishwe mahakamani.
Tukio la kuawa kwa mfanyakazi wa Tanesco limewashtua wakazi wengi wa mkoa huo akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Waziri Kindamba ambaye aliwaagiza polisi wawasake wahusika kwa udi na uvumba.


Chanzo: Mwanachi
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages