Breaking

Wednesday 18 January 2023

NGOs ZAKUMBUSHWA KUFUATA MISINGI YA KATIBA, KANUNI NA SHERIA



Na WMJJWM, Dodoma

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yametakiwa kufuata misingi ya katiba, sheria na kanuni zilizowekwa katika utekelezaji wa majukumu Yao.

Akizindua Bodi ya 5 ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, jijini Dodoma leo Januari 18, 2023, Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka Bodi hiyo kusimamia vema uendeshaji wa Mashirika hayo kuanzia ngazi za chini na kufungamanisha taarifa za utekelezaji wa NGO na taarifa za serikali zinazowasilishwa ngazi zote Ili jamii ione tija ya utekelezaji wa NGO na kushirikiana zaidi.

Amesema NGO’s ni wajumbe wa kamati mbalimbali zinazohusika kusukuma ajenda za serikali mfano katika kupambana kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto hivyo, NGO zina haki ya kupaza sauti kwenye Bodi ya NGO iwapo hakuna ufanisi wa kamati na NGO zipo Ili kusaidia. Lengo ni wadau kuisadia serikali na Serikali kuziwezesha NGO kutimiza wajibu wao na wananchi kunufaika.

“Kuna baadhi ya Mashirika yanaendesha shughuli zao kinyume na Sheria za nchi, hivyo mje na njia ya kupata Taarifa. NGOs ziko nyingi zinazofanya kazi Nzuri lakini zipo ambazo zinafanya mambo ambayo hayaendani na Tamaduni zetu, mchukue hatua” Alisisitiza Dkt Gwajima.

Aidha Dkt Gwajima ameipongeza Bodi iliyopita na kuwaagiza kuendelea kutoa ushirikiano kwa wajumbe wa Bodi mpya na kumpongeza Mwenyekiti Bi Mwantumu na Wajumbe wote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi Bi Mwantumu Mahiza amemshukuru Raise Samia Suluhi Hassan kwa kumuamini kusimamia chombo hicho muhimu na kuwasisitiza Wajumbe wateule kujipanga kuhakikisha NGOs zinafanya kazi inavyoonekana.

Bi. Mahiza amesema atasimamia Bodi kuhakikisha NGOs zinafanya kazi kwa kufuata kanuni na sheria za nchi kwa kuona kila shirika linafanya nini.

"Umuhimu wa chombo hiki ni kuhakikisha Mashirika yanafanya kazi zinazoonekana, lakini kuna uharaka unahitajika wa sisi kama Bodi kupitia sheria, sera na kanuni ili tuone kama zinaendana na matakwa ya nchi na wakati tulio nao" amesema Mwantum.

Naye Mbunge wa viti maalum mwakilishi wa NGOs Mhe. Neema Lugangira ameiomba Serikali kupitia Bodi hiyo kuangalia baadhi ya Changamoto ambazo zimeendelea kufanya Bodi kushindwa kufanya kazi inavyotakiwa ikiwemo ushirikishwaji kwenye vikao vya kisekta.

“Changamoto nyingine ni Upatikanaji wa Vibali kwa muda ili kusaidia Mashirika kuweza kufanyia kazi zao za kuwafikia Wananchi kwa uharaka zaidi”Alisema Neema Lugangira.

Uzinduzi wa Bodi hiyo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri Mhe. Mwanaidi Ali Khamis na Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula.




MWISHO
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages