Breaking

Tuesday 24 January 2023

POLISI WAUA MAJAMBAZI WAWILI KAGERA


JESHI la Polisi mkoani Kagera limewaua watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika Kijiji cha Kumunazi wilayani Ngara mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, William Mwampaghale amesema, watuhumiwa hao wanakadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 na 30, lakini majina yao bado hayajatambulika, ila miili imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Nyamihaga wilayani Ngara.

Amesema, Januari 21, 2023, polisi walipata taarifa kuwa kuna kundi la wahalifu wanaotumia pikipiki linapanga kufanya uhalifu kati ya barabaraba ya Kumunazi na Rulenge, ambapo majira ya saa 3:35 polisi liliweka mitego mbalimbali na kufanikiwa kunasa wahalifu hao, ambao walikufa katika kurushiana risasi.


Kamanda Mwampaghale amesema, katika mtego wao ilipita pikipiki waliyoihofia ambayo ilikuwa imebeba watu watatu,polisi waliisimamisha pikipiki hiyo lakini haikusimama, wakafyatua risasi juu, lakini bado waliendelea kukimbia.

Amesema, waliwakimbiza lakini walikaidi na kuanza kurushiana risasi, ambapo mmoja alijeruhiwa mguuni na mwingine kiunoni na hali zao zilikuwa mbaya wakati wakikimbizwa Hospitali ya Nyamihaga.

Hata hivyo, amesema, mara baada ya kufanya upekuzi kwenye makoti waliyokuwa wamevaa, walikutwa wakiwa wamebeba bunduki aina ya AK47, ikiwa na risasi 25 pamoja na mabomu mawili ya kurusha kwa mkono.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages