Breaking

Saturday 21 January 2023

RAIS DKT. MWINYI ATEUA VIONGOZI SITA




RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewateua viongozi mbalimbali.

Kupitia taarifa iliyotolewa Ijumaa Januari 20, 2023 na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Mhandisi Zena A.Said imeeleza kuwa Rais Dkt.Mwinyi amemteua ndugu Samora John Chacha kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale.

Kabla ya uteuzi huo Chacha alikuwa ni mfanyakazi wa sekta binafsi.

 Rais Dkt.Mwinyi amemteua Adil Fauz George kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Uratibu wa Shughuli za Utalii katika Kamisheni ya Utalii ambapo Kabla ya uteuzi huo, Adil alikuwa ni mfanyakazi wa sekta binafsi.

Yakout Hassan Yakout ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma, ndugu Yakout ni Katibu Mkuu mstaafu.

 Ali Saleh Mwinyikai kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Magazeti ambapo kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndugu Ali ameteuliwa kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha pili.

Bibi Safia Ali Rijaal kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Huduma za Maktaba Zanzibar huku taarifa ikieleza kuwa Bibi Safia ni mstaafu katika utumishi wa umma. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo unaanza Januari 20, 2023.

Aidha Rais Dkt.Mwinyi amemteua Ussy Khamis Debe kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu ambapo kabla ya uteuzi huo Ussy alikuwa Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar na uteuzi wake umeanza Desemba 30,2022.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages