Breaking

Tuesday 31 January 2023

SERIKALI YATOA MIKOPO BILIONI 165 KWA WAKULIMA


Na. Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mkopo wa shillingi billioni 164.9 kwa Sekta ya Benki na Taasisi za Fedha nchini uliowanufausha wakulima wadogo 5,385 na Vyama vya Ushirika na Masoko (AMCOS) 21.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Halima Mdee aliyetaka kujua makundi yaliyonufaika na mkopo wa shilingi trilioni moja iliyoahidiwa kutolewa na Serikali katika sekta ya kilimo pamoja na masharti yake.

Mhe. Nchemba alisema utoaji wa mkopo huo ambao takwimu zake zinaishia tarehe 31 Disemba 2022, ulikuwa ni utekelezaji wa hatua za ziada za kisera zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo kuanzisha mkopo maalum wa shilingi trilioni moja kwa benki na taasisi za fedha nchini ili kuchochea mikopo nafuu kwa Sekta Binafsi hususan Sekta ya Kilimo.

Alisema Masharti ya mkopo huo maalum yalikuwa kuchochea mnyororo wa thamani katika kilimo cha mazao, miundombinu ya umwagiliaji, mifugo, uvuvi na ununuzi na usindikaji wa mazao yake kwa wakulima wadogo na wa kati pamoja na kampuni ndogo ndogo na za kati (SMEs).

“Masharti mengine ni Benki Kuu kuzikopesha benki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia tatu, ili taasisi hizo ziwakopeshe wakulima na kampuni zinazojishughulisha na mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10”, alifafanua Mhe. Nchemba.

Aidha, alibainisha kuwa benki na taasisi za fedha zinatakiwa kutoa mkopo usiozidi shilingi bilioni moja kwa kila mkulima kwa riba ya chini ya asilimia 10.

Alieleza kuwa kasi ya utoaji wa mikopo hiyo inategemea na mahitaji ya Sekta ya fedha zikiwemo Sekta za fedha na kuwahimiza Wabunge kuwashawishi wananchi kuchangamkia fursa hiyo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages