Breaking

Monday 23 January 2023

TAKUKURU YATAKIWA KUTOA MAFUNZO PROGRAMU YA TAKUKURU RAFIKI KWA WATENDAJI WA KATA



Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoa mafunzo kwa watendaji wa kata kuhusu utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini, ambavyo vimekuwa ni kikwazo cha maendeleo katika taifa.

Mhe. Chaurembo ametoa maelekezo hayo january 22, 2023 jijini Dodoma, wakati Kamati yake ya USEMI ikipatiwa mafunzo na TAKUKURU kuhusu Programu ya TAKUKURU RAFIKI, ambayo yaliyolenga kuwajengea uelewa wa program hiyo wajumbe wa kamati hiyo ili washirikiane na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mhe. Chaurembo amesema, moja ya jukumu la Watendaji Kata ni kuwasaidia Wakurugenzi na Watendaji wengine kuleta maendeleo katika ngazi ya Kata, hivyo wakiielewa vema programu ya TAKUKURU RAFIKI itawasaidia kwenye eneo la usimamizi wa miradi katika sekta kipaumbele za afya, maji, elimu, kilimo, ardhi na miundombinu.

“TAKUKURU ni wajibu wenu kuhakikisha Watendaji wa Kata wanapatiwa mafunzo ya Programu ya TAKUKURU RAFIKI ili waweze kuwaunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema TAKUKURU RAFIKI ni programu iliyotokana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliielekeza TAKUKURU kuandaa programu itakayoiwezesha kuzuia vitendo rushwa badala ya kupambana navyo.

Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya USEMI ya kutoa elimu kwa Watendaji wa Kata kuhusu Programu ya TAKUKURU RAFIKI, Mhe. Ndejembi amesema TAKUKURU itaenda kwenye ngazi ya Kata kutoa elimu hiyo kwa watendaji hao ikiwa ni pamoja na wananchi ili kila mwananchi aweze kuwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.

Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye amesema taasisi yake ina ari, azma na nia ya kuhakikisha kwamba rushwa inatokomezwa nchini Tanzania kupitia Programu ya TAKUKURU RAFIKI.

Akizungumzia mwitikio wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa, Bi. Mwakalyelye amesema asilimia 92 ya wananchi wameonesha utayari wa kushiriki mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika taifa, hivyo Programu ya TAKUKURU RAFIKI itatumika kikamilifu kuitokomeza rushwa.

Aidha, Bi. Mwakalyelye ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) kwa maelekezo na maoni iliyoyatoa na kuahidi kuyafanyia kazi ili TAKUKURU itekeleza jukumu lake la msingi la kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Programu ya TAKUKURU RAFIKI ilianzishwa kwa lengo la kuongeza ushiriki wa mwananchi na wadau katika kukabiliana na tatizo la rushwa kwenye eneo la utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages