Breaking

Sunday 19 February 2023

SERIKALI KUONDOA CHANGAMOTO WAZALISHAJI CHUMVI



Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesisitiza kuwa, Serikali inawathamini wazalishaji wa Chumvi hapa nchini ili kuongeza uzalishaji wa chumvi kwa kuhakikisha kuwa inaondoa changamoto zote zinazokwamisha maendeleo katika Sekta ya Madini kuwawezesha wachimbaji wa madini wafanye shughuli za uchimbaji madini kwa tija.

Dkt. Kiruswa amesema hayo Februari 18, 203 alipotembelea eneo la machimbo ya chumvi la Chakulu wilayani Uvinza mkoa wa Kigoma ili kuzungumza na kikundi cha Kinyo Farmers and Salt Works na Kikundi cha Twikome Salt Kinyo Chakulu.

"Ninasisitiza kuondoa migogoro katika eneo hili ili kuchochea ongezeko la uzalishaji wa Chumvi hapa nchini ili wachimbaji wanufaike na rasilimali hii muhimu," amesisitiza Dkt. Kiruswa.

Katika hatua nyingine, Dkt Kiruswa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Uvinza kwa Kushirikiana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kigoma afanye kikao na Wamiliki wa leseni na Àrdhi siku ya Jumatatu tarehe 20/02/2023 kwa ajili ya kuandika makubaliano yaliyofanyika katika mkataba.

Aidha, ameiagiza Tume ya Madini kushirikiana na Taasisi ya Jiolijia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutembelea maeneo ya leseni za vikundi vyote ili kubainisha maeneo ambayo yanaweza kuchimbwa visima vya kuzalishia Chumvi.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kigoma Mhandisi Pius Lobe amevitaka vikundi hivyo wakubaliane ili kuondoa migogoro waliyonayo. Aidha amewataka kufuata maelekezo yaliyotolewa na Dkt. Kiruswa ili kuendelea na uzalishaji.

Vile vile, Meneja wa Leseni wa Tume ya Madini, Samwel Mayuki amewataka wamiliki wa leseni na wamiliki wa ardhi kukubaliana na pendekezo la kuingia makubaliano ili kuepuka kusitishwa kwa shughuli za uzalishaji wa chumvi endapo mgogoro huo utaendelea au kutakiwa kufanyika kwa fidia ya ardhi.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini Nashoni Bidyanguze amemshukuru Dkt. Kiruswa kwa kufika kutatua mgogoro huo wa chumvi ambao umechukua muda mrefu. Amesisitiza Serikali kuboresha machimbo hayo ili kuongeza uzalishaji wa chumvi, kuongeza mapato ya Serikali na wananchi kupata ajira.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages