Breaking

Tuesday 14 February 2023

MCHANGO WA SEKTA YA MADINI PATO LA TAIFA WAFIKIA ASILIMIA 9.7



Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wadau wa sekta ya Madini ili kuiwezesha sekta hiyo kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo Mwaka 2025 ambapo mpaka sasa mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa umeongezeka na kufikia asilimia 9.7.

Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya kisekta kati ya Wizara ya Madini na wadau wa sekta Madini kuhusu changamoto na fursa zilizopo katika sekta hiyo ikiwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwa watendaji wa wizara hiyo.

“Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuiwezesha sekta ya Madini kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025 kwa kuondoa changamoto zote zinazowakabili wachimbaji wa madini nchini ili kuwezesha shughuli hiyo kuendelea kukuwa na kukuza uchumi nchini ambapo mpaka sasa mchango wa sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka na kufikia asilimia 9.7” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko amesema ili kuhakikisha sekta hiyo inaimarika, Serikali imefuta leseni za maeneo ya uchimbaji yasiyoendelezwa ili kuyagawa upya kwa wachimbaji wengine wenye nia ya kufanya shughuli za uchimbaji madini.

Amesema hatovumilia kuona baadhi ya wachimbaji wakikwamisha sekta hiyo hasa wale ambao wamepewa leseni na hawaendelezi shughuli za uchimbaji kwani serikali imeanza kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuzifuta leseni zisizo endelezwa.

"Hadi sasa tumezifuta zaidi ya leseni 7,000 zilizokuwa zikimilikiwa na watu ambao wameshindwa kuziendeleza na hatua hiyo imekuja baada ya serikali kubaini changamoto kwa baadhi ya wachimbaji wadogo kuvamia leseni za watu wengine,” amesema Dkt. Biteko.

Kwa Upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Adolf Ndunguru amesema serikali imezichukua changamoto zote zilizotolewa na wadau wa sekta ya Madini na kuahidi kuzifanyia kazi ikiwemo mrundikano wa tozo, leseni zisizoendelezwa n.k ili kurahisisha shughuli za uchimbaji nchini.

Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga amesema mkutano huo utaiwezesha sekta ya Madini kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi nchini.

“Mkutano huu umelenga kujadili changamoto za wachimbaji wa madini wanazokabiliana nazo ambazo ni za kodi kuwa kubwa, leseni na wachimbaji wadogo kuvamia maeneo ya wachimbaji wakubwa lengo likiwa kufikia mapendekezo ya kuendeleza ukuaji wa uchumi nchini,” amesema. Dkt. Wanga.

Awali baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo wamesema kuwa kuondolewa kwa changamoto hizo itasaidia kuleta maendeleo kwenye sekta ya Madini na kuchangia zaidi ya asilimia 10 kwenye Pato la Taifa kama iliyokusudiwa na Serikali.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages