Breaking

Tuesday, 21 February 2023

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MKE WA MWENYEKITI AKAMATWAJeshi la Polisi Mkoa wa Kagera limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa mauaji PASCHAL KAIGWA MARISELI (21) aliyekuwa akitafutwa kwa kosa la mauaji ya HADIJA ISMAIL (29) mkazi wa mtaa wa National Housing, Kata ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba Mkoa wa Kagera.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Kagera ACP William Mwampaghale imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo alitoroka mara baada ya kutekeleza mauaji tarehe 13/02/2023 na kwenda kujificha katika vichaka kwa muda wote huo.

Soma pia: MKE WA MWENYEKITI ABAKWA NA AUAWA

Kamanda Mwampaghale amesema mnamo tarehe 19/02/2023 majira ya saa 10:00 alitoka mafichoni baada ya njaa kali na kuamua kwenda kutafuta msaada wa chakula nyumbani kwa shangazi yake katika mtaa wa Kashai Katotorwansi manispaa ya Bukoba.

"Huko aliwakuta watoto wa shangazi yake ambao wanamfahamu na baada ya kumuona ndipo walipiga kelele majirani wakafika na kumkamata kwakuwa tayari tukio alilofanya lilikuwa limeshatangazwa na vyombo vya habari na Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera lilishatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pale mtuhumiwa huyo atakapoonekana kwenye maeneo yao."

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashukuru wananchi wote wa mkoa wa Kagera na linatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano wao kufichua wahalifu na vitendo vya uhalifu liweze kuchukua hatua ya kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili kuepuka vitendo vya ukatili na mauaji katika jamii yetu." Ameeleza ACP Mwampaghale

Soma pia: MKE WA MWENYEKITI ABAKWA NA AUAWA

Aidha Kamanda Mwampaghale ametoa onyo kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu ikiwemo mauaji, ubakaji na ukatili kuacha mara moja na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote wanaofanya vitendo hivyo vya kihalifu ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages