Breaking

Sunday 12 February 2023

ASKARI UHIFADHI WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka Askari wa Uhifadhi katika maeneo mbalimbali nchini wazingatie sheria kanuni,taratibu na miongozo pindi wanapotekeleza majukumu yao ikiwemo kulinda Maliasili.

Ameyasema hayo Februari 11, 2023 Wilayani Ushetu Mkoani Shinyanga mara baada ya kutembelea Kata ya Mlowa wakati wa ziara yake kikazi yenye lengo la kutatua changamoto baina ya wananchi na wahifadhi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka wananchi wake waishi kwa amani bila taharuki ya aina yoyote, hivyo Askari wa Uhifadhi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya sheria.

“Sisi tumepewa dhamana ya kusimamia maliasili kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo, katika kutekeleza jukumu hili hatupaswi kuleta taharuki kwa wananchi” amesisitiza Mhe. Mary Masanja.

Amewaeleza wananchi hao kuwa mtu yeyote anapovunja sheria kwa kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa bila vibali lazima utaratibu wa kisheria ufuatwe ikiwemo kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Aidha, ametoa rai kwa wananchi hao waendelee kufuata sheria na kuacha kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuwa maeneo hayo ni muhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Pia, amewataka Askari Uhifadhi waandae programu za kutoa elimu kwa wananchi ili wajue umuhimu na faida za uhifadhi ikiwemo kuleta mvua, kutunza vyanzo vya maji,kuchavusha mazao na kusaidia katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi.

Naye,Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita amesema ataendelea kushirikiana na wahifadhi kuhakikisha elimu ya uhifadhi inaendela kutolewa kwa wananchi wanaozunguka Pori hilo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages