Breaking

Wednesday 8 February 2023

SERIKALI YABAINISHA MIKAKATI KUPAMBANA NA FISTULA



Na WAF- Dodoma

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha mikakati ya Wizara ya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Fistula, ikiwemo kutoa elimu dhidi ya mimba za utotoni na kuwaelemisha akinamama kuhudhuria kliniki mapema.

Dkt. Mollel amesema hilo leo Februari 08, 2023 wakati akijibu swali la Mhe. Aleksia Kamguna katika Mkutano wa kumi kikao cha saba, Bungeni Jijini Dodoma.

"Katika kupambana na ugonjwa huu wa Fistula Serikali imekuwa ikitoa elimu kuhusu mimba za utotoni kupitia elimu ya uzazi kwa vijana na kuwaelemisha akinamama kuhudhuria kliniki mapema." Amesema Dkt. Mollel.

Ameendelea kusema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa elimu kwa wajawazito kujifungulia katika vituo vya huduma ili kuwahi kupatiwa msaada kama kutatokea tatizo la uchungu pingamizi au jingine.

Sambamba na hilo, Dkt Mollel amesema, Serikali imeendelea kutenga fedha kwaajili ya kuboresha miundombinu na huduma katika vituo vyote nchini vya kutolea huduma za afya nchini ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema, kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 kwa kimetolewa kwaajili ya upanuzi wa miundombinu ya majengo ya huduma za Dharura, Huduma za Wagonjwa Mahututi, Huduma za Mionzi katika hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

Ameendelea kusisitiza kuwa, tayari ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.8, umefanyika katika hospitali hiyo huku kiasi cha shilingi Milioni 350 kikitolewa kwaajili ya umaliziaji wa jengo la upasuaji wa mifupa (Orthopedic theatre) ambapo jengo hili litakamilika mwezi Juni, 2023.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages