Breaking

Wednesday 8 March 2023

RAIS SAMIA AHUTUBIA BARAZA LA WANAWAKE WA CHADEMA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Maridhiano kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mhe. Freeman Mbowe aliyeikabidhi kwa niaba ya Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) mara baada ya kuwahutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Moshi Mkoani Kilimanjaro tarehe 08 Machi, 2023.
****************

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema muda sio mrefu ataunda kamati kwa kushirikiana na vyama vingine vya siasa ambayo itashughulika na suala la katiba mpya.

Akizungumza leo Machi 8, 2023 kwenye Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani wa Chadema, Rais Samia amesema suala hilo hakuna anayelipinga.

“Swala katiba hakuna anayekataa hata chama changu hakuna anayekataa, na muda si mrefu tutatangaza kamati ambayo itashughulikia jambo hilo”.amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo wa nchi amesema kuwa “Hakuna kisichowezekana kwa mazungumzo, tulishuhudia nchi kadhaa ziliingia kwenye vita hakukupatikana suluhu, lakini suluhu ikaja kupatikana kwa mazungumzo”.


Aidha Rais Samia amekataa kukubali ombi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuingilia kati sakatala la wabunge viti maalum 19, wanaodaiwa kuwepo bungeni kinyume cha sheria, akisema suala hilo liko mahakamani.


Ni baada ya baraza hilo na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, kumuomba aingilie kati ili wabunge hao waondolewe bungeni kwa madai kuwa hakijawateua.

“La mwisho kwa jina mliloliita (Covid-19), wote wawili wamesema japo kwamba lipo mahakamani lakini mama…, niwaambie tuache mkondo ule uendelee tutazame mbele yanayokuja. Tuachie mkondo ule uendelee, si rahisi mimi hata kama ni Rais kutia mkono huko,” amesema Rais Samia.

Wabunge hao wakiongozwa na Halima Mdee, walifungua kesi Na. 36/2022 katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, kupinga uamuzi wa Chadema kuwavua uanachama kwa tuhuma za usaliti kufuatia uamuzi wao wa kwenda kuapishwa bungeni jijini Dodoma, kuwa wabunge viti maalum.

Katika kesi hiyo inayosikiliwa mbele ya Jaji Cyprina Mkeha, Mdee na wenzake wanadai hawakujipeleka bungeni, bali waliteuliwa na uongozi wa chama hicho, hivyo wanaiomba mahakama ifanye mapitio dhidi ya mchakato uliotumika kuwavua uanachama wakidai haukuwa halali.

Kwa sasa kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mahakamani hapo, ambapo kesho tarehe 9 Machi 2023, mawakili wao wataanza kuwahoji baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Chadema, akiwemo Dk. Azaveli Lwaitama, dhidi ya hati zao za viapo kinzani walizowasilisha mahakamani kujibu malalamiko ya wabunge hao kufukuzwa kinyume cha sheria.



Viongozi mbalimbali wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) pamoja na Wanachama wa Chama hicho wakishangilia wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia katika Mkutano wa Baraza hilo uliofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi, 2023.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages