Breaking

Monday 20 March 2023

WAZIRI BITEKO ATAKA BAJETI YA 2023/24 KUZINGATIA VIPAUMBELE VYA WIZARA



*Katibu Mkuu Mahimbali asema kumekuwa na utekelezaji mzuri wa malengo ya mwaka 2022/23*


*Dkt. Kiruswa ataka watumishi kuimarisha ushirikiano*


*TUGHE waeleza wameshuhudia mafanikio makubwa Sekta ya Madini*


*Dodoma*


Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka Watumishi wa Wizara ya Madini kuhakikisha Bajeti iliyopangwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 inazingatia uimarishaji wa ukusanyaji maduhuli ili kufikia lengo la kuchangia asilimia10 kwenye Pato la Taifa.


Aidha, amewataka watumishi na wataalam wa wizara kuweka nguvu katika uendelezaji wa madini ya kimkakati, uendelezaji wa wachimbaji wadogo, uongezaji thamani madini na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara.


Waziri Biteko ameyasema hayo Machi 19, 2023, wakati akifungua Mkutano wa baraza la Wafanyakazi Wizara ya Madini ambalo pia lilihudhuriwa na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya wizara na wawakilishi kutoka Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Makao Makuu.


Aliongeza kwa kumwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Madini kusimamia fedha zinazopatikana kutekeleza majukumu yaliyopangwa kwa kuzingatia vipaumbele vya wizara bila kusahau haki na stahili za watumishi kwa kuwa ustawi wao ndio nguzo katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.


Aidha, Waziri Biteko alitumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa wizara na kueleza kuwa, pamoja na kuwepo changamoto za kibajeti, hali hiyo haijawazuia kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao. Kufuatia hali hiyo, amewataka kuhakikisha wanatekeleza majukumu kwa tija na kutoa matokeo chanya ambayo yatapelekea kupatiwa fedha za kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali akizungumza katika mkutano huo pamoja na mambo mengine  alisema  kumekuwa na utekelezaji mzuri wa malengo  yaliyowekwa na wizara kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023  ambayo yamepelekea  kuwepo mafanikio kadhaa ikiwemo ongezeko la mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa kwa robo ya Tatu ya Mwaka 2022 (Julai – Septemba 2022) hadi kufikia asilimia 9.7 ikilinganishwa na asilimia 7.9 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021


Aidha, ameyataja mafanikio mengine kuwa ni ongezeko la makusanyo ya maduhuli yaliyokusanywa na kuwasilishwa Hazina kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Februari 2023 hadi kufikia shilingi bilioni 457.23 ikilinganishwa na shilingi bilioni 412.09 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/22.


 Vilevile, alisema marekebisho ya sheria na kanuni zimewezesha kurasimisha shughuli za uchenjuaji wa madini na kuiwezesha Serikali kujua mashapo kupitia tafiti za GST na kufanya majadiliano yenye tija na kampuni za madini ambazo Serikali inashiriki katika ubia.


Awali, akitoa salam  katika mkutano huo Mwakilishi kutoka TUGHE Makao Makuu   Nsubisi Mwasandende alisema Chama kitaendelea kushirikiana na wizara na kueleza kuwa, TUGHE imeshuhudia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Sekta yaMadini


Naye, Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Madini Joseph Ngulumwa amesema  watumishi wizara ya madini wanajivunia uongozi wa wizara kutokana na namna unavyosimamia utekelezaji wa majukumu ya wizara na watumishi na kueleza kuwa, TUGHE wizarani itaendelea kushirikiana na wizara.


Akifunga mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesisitiza watumishi kushirikiana kwa karibu ikiwemo kubadilisha taarifa ambazo zitawezesha kutekelezwa kikamilifu kwa majukumu ya Wizara.


Mkutano huo umetoka na maazimio kadhaa ikiwemo masuala ya uendelezaji wa madini ya kimkakati.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages