Breaking

Sunday 21 May 2023

MCHENGERWA ATOA MIEZI MIWILI KUKAMILISHA MKAKATI ACHIA SHOKA KAMATA MZINGA, AZINDUA MWONGOZO WA USIMAMIZI WA HIFADHI ZA NYUKI


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka watendaji wa sekta ya Misitu na Nyuki kukamilisha mkakati wa kuongeza uzalishaji wa asali toka tani 35000 za sasa hadi tani 138000 katika kipindi cha miezi miwili alioupa jina la mkakati wa “achia shoka kamata mzinga” huku akitaka eneo la misitu na asali kufanyiwa utafiti wa kutosha ili litumike kama zao jipya la utalii.


Mhe Mchengerwa ameyasema hayo leo Mei 21, 2023 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Bombadia mkoani Singida.

Akiwa kiwanjani hapo amezindua Mwongozo wa Usimamizi wa Hifadhi za nyuki, na vibanda maalum vya kuuzia asali pia ametoa Tuzo 5 za wadau wenye mchango mkubwa kwenye Sekta ya nyuki na ametoa vyeti kwa wanafunzi walioandika nsha nzuri kuhusu ufugaji wa nyuki.


Akisoma hotuba yake amesema pamoja na uwepo wa maeneo makubwa yaliyohifadhiwa na yanayofaa kwa ajili ya kuzalisha mazao ya nyuki yenye viwango bora vado takwimu zinaonesha uzalishaji ni 23% ikilinganishwa na uwezo uliopo wa kuzalisha tani 138,000 kwa mwaka.

Kutokana na hali hiyo Mhe. Mchengerwa ameelekeza Wizara ya Maliasili ishirikiane na Wizara ya Kilimo kuanzisha programu za matumizi ya makundi ya nyuki kwenye uchavushaji mimea ili tuweze kuongeza kiwango na ubora wa mazao yanayozalishwa.

Ameitaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu kuhakikisha wanawezesha wananchi hasa wale wanaopakana na maeneo ya hifadhi kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na mizinga ya kisasa. Pia kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha jamii kupanda na kuitunza miti katika maeneo yao.

Aidha, amesema pamoja na Serikali kuweka jitihada kubwa kwenye kulinda na kuhifadhi maliasili, bado katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na kasi kubwa ya uharibifu wa maeneo yaliyohifadhiwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Akitolea mfano amesema mkoa wa Singida umebarikiwa kuwa na uoto wa kipekee ujulikanao kwa jina maarufu kama Vichaka vya Itigi (Itigi Thicket) ambao upatikana katika nchi mbili tu duniani, yaani Tanzania na nchi ya Zambia ambao katika kipindi cha miaka kumekuwa na kasi kubwa ya ukataji na uondoaji wa uoto huu kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Hali hii imesababisha sehemu kubwa ya ardhi iliyokuwa na uoto huu kubaki wazi na pia kumebainika kuwepo kwa mimea vamizi pale ambapo uoto huu ulipoondolewa. Kutokana na hali hiyo ameielekeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyobaki ambayo yenye uoto huo yanatambuliwa na kuhifadhiwa kisheria, pia wananchi waliopo kwenye maeneo hayo wanapewa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira na ufugaji nyuki kibiashara.


Ameitaka TFS kuhakikisha vijiji vyote vya maeneo hayo vinakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi na inatekelezwa ipasavyo.


Pia kutoa elimu kwa wafugaji nyuki ili waweze kutumia vifaa sahihi vitakavyoweza kuendeleza uhifadhi wa maeneo hayo.

Akizungumzia kuhusu zoezi la uwekaji wa mizinga nchi nzima Mhe Mchengerwa ametoa rai kwa wananchi kutumia wataalamu wa ufugaji nyuki waliokwenye maeneo yao kupata elimu sahihi ya namna ya kufuga nyuki kwa tija na kusisitiza wataalamu watoke maofisini na kwenda kuwahudumia wananchi.


Aidha amesema pamoja na faida nyingi tunazopata kutoka kwa mdudu nyuki bado nyuki anaweza kutumika kutupatia zao jipya la utalii ambapo amesema katika nchi ya Solvenia mdudu nyuki hutumika sana kwa ajili ya shughuli za utalii.


Amewataka wataalamu kuangalia namna watakavyoweza kupata sifa za kipekee za asali inayozalishwa hapa nchini ili tuweze kuitangaza Kimataifa ambapo ametoa wito kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine; pamoja na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela Arusha kufanya utafiti huu.


Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akielekeza na kusisitiza kulinda Maliasili na kuendeleza utalii.


Aidha, amempongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohammed Mchengerwa (Mb) kwa kutembea takriban nchi nzima kuhamasisha utunzaji wa maliasili, mazingira na uendelezaji utalii.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: + 255 621 615 613 au +255 621 896 990

Pages